Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu laanza rasmi mjadala wa wawakilishi wote

Baraza Kuu laanza rasmi mjadala wa wawakilishi wote

Ijumanne, tarehe 25 Septemba (2007) wajumbe wa kimataifa walianza rasmi mahojiano ya mwaka kwenye kikao cha wawakilishi wote kilichofanyika kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la UM. Kikao cha mwaka huu ni cha 62, na wajumbe kutoka Mataifa Wanachama kadha wa kadha waliwasilisha sera zao za kitaifa kuhusu hatua wanazochukua kukabiliana na matatizo yanayosumbua walimwengu.~~Raisi mpya wa Baraza Kuu, Srgjan Kerim, kutoka Jamhuri ya Yugoslavia ya Zamani ya Macedonia pamoja na KM wa UM, Ban Ki-moon walijumuika na viongozi mbalimbali wa Nchi Wanachama kuzingatia taratibu za kuchukuliwa kipamoja kustawisha uhusiano mwema wa kimataifa.

Risala ya KM Ban Ki-moon kwenye kikao cha ufunguzi cha Baraza Kuu ilipendekeza Mataifa Wanachama yajumuike kusaidia “kuongeza nguvu kazi kwenye taasisi yetu ya kimataifa ili kukuza maendeleo na kuimarisha amani kote ulimwenguni.” Raisi George Bush wa Marekani yeye alisema anaunga mkono kazi za UM katika kukabiliana na matatizo sugu yanayoutatanisha ulimwengu. Raisi wa Baraza Kuu, Srgjan Kerim risala yake ilitilia mkazo zaidi ulazima wa kuhamasisha walimwengu kutunza mazingira ili tuweze kudhibiti vyema mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni. Kulingana na rai hiyo, Raisi Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil alipendekeza kuitishwe mkutano mkuu wa kimataifa katika 2012 kuzingatia namna ya kushirikiana kimataifa kudhibiti vyema mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Raisi wa Ufaransa Nicolas Sarkozy yeye alitaka UM uanzishe “mfumo mpya” wa kazi zake utakaokuwa na maadili ya haki. Lakini Raisi Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, akiwakilisha msimamo wa, takriban, fungu kubwa la mataifa ya Afrika, alionya kwamba nadharia alionayo inaonesha mataifa makuu huwa yanapotosha kazi za taasisi za ushirikiano wa kimataifa, mathalan UM, ambapo mara nyingi mataifa makuu hushikilia kusukuma mbele zaidi masilahi yao badala ya masilahi ya umma wote wa kimataifa. Raisi Robert Mugabe wa Zimbabwe alisisitiza kuwa wakati umeshawadia kihistoria ‘kuhuisha tena’ na kufufua shughuli halali za Baraza Kuu ili hatimaye Baraza hilo liweze kuwakilisha kihakika matakwa ya umma wa kimataifa. Wawakilishi wa mataifa ya visiwa vya Bahari ya Pasifiki hootuba zao zilihimiza nchi tajiri kufidia mataifa masikini misaada itakayoyawezesha kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa yanayochochewa na maisha ya ubadhirifu ya mataifa yenye maendeleo ya viwandani.

Hiyo wasikilizaji ilikuwa ni kumbukumbu ya baadhi ya maoni ya nchi wanachama yaliowasilishwa kwenye wiki ya awali ya mijadala ya wawakilishi wote katika Baraza Kuu, mijadala ambayo inatazamiwa kuendelea Makao Makuu hadi tarehe 03 Oktoba 2007.