Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama latathminia amani na usalama wa Afrika

Baraza la Usalama latathminia amani na usalama wa Afrika

Viongozi wa Kitaifa, wakijumuika na wakuu wa Serekali pamoja na mawaziri wa vyeo vya juu kutoka nchi 15 zilizo wanachama wa Baraza la Usalama, pamoja na KM wa UM Ban Ki-moon na Mwenyekiti Alpha Oumar Konare wa Umoja wa Afrika (AU) walikusanyika mapema wiki hii kwenye Baraza la Usalama kujadilia njia bora za kurudisha utulivu wa amani na usalama katika Afrika, eneo ambalo linadaiwa kuwa na vurugu na migogoro ya kila aina.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Alpha Oumar Konare yeye aliwakumbusha wajumbe wa Baraza la Usalama umuhimu wa kukuza ushirikiano mwema na jumuiya ya kimataifa. Hata hivyo, licha ya kuwa Umoja wa AU unahitajia kufadhiliwa misaada ilioahidiwa siku za nyuma na jumuiya ya kimataifa, kuweza kuhudumia mahitaji yake, inafaa pia ikumbukwe na wadau wenzi wanaoshirkiana na Afrika kwamba haiwafalii wao hata kidogo kuendeleza tabia ya kuingilia kati, kulikopita kiasi, mambo ya ndani ya Afrika. Alikumbusha tena kwamba enzi za ukoloni hazipo tena, zimeshapitwa na wakati kitambo sasa.

Raisi wa Afrika Kusini Thabo Mbeki, alipohutubia kikao cha Baraza la Usalama alikumbuha kwamba mjadala umeweza kufanyika kwa sababu ya hatua zilizokwishachukuliwa na mataifa ya Afrika wenyewe, katika kuwasilisha suluhu kwenye ile migogoro iliofumka Cote d’Ivoire, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na maeneo mengine yaliokabiliwa na matatizo. Alinasihi kwamba ushirikiano muhimu unaohitajia kuimarishwa kati ya UM na Afrika sasa hivi ni ule wa kuisaidia Afrika kuwa na uwezo imara unaohitajika kukabiliana na masuala sugu yaliolipamba bara hilo. Alisisitiza Raisi Mbeki kwamba kilichokosekana katika usanifu wa mradi wa kutaka kuisaidia Afrika kujipatia utulivu na amani inayolingana na mahitaji yake ya kikanda ni rasilmali ya kutegemewa, na uwezo wa kuyatekeleza, kama inavyopaswa, malengo ya kuimarisha amani kijumla.