Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM azungumza na waandishi habari juu ya ziara yake ijayo katika Sudan, Chad na Libya

KM azungumza na waandishi habari juu ya ziara yake ijayo katika Sudan, Chad na Libya

Ijumanne, Agosti 28 (2007) Katibu Mkuu (KM) wa Umoja wa Mataifa (UM) Ban Ki-moon alikuwa na mazungumzo na waandishi habari katika Makao Makuu juu ya ziara yake katika mataifa ya Chad, Libya na Sudan kusailia kipamoja na viongozi wa mataifa haya juu ya taratibu zitakazosaidia kurudisha utulivu na suluhu ya kuridhisha kuhusu tatizo la Darfur. KM alianza mazungumzo kwa kuelezea sababu hasa zilizomhamasisha yeye binafsi kuamua kufanya ziara hii:

"Ningependelea kwenda kwenye eneo husika, kujionea mwenyewe ile hali ngumu ya kimazingira itakayowakabili wanajeshi wa vikosi vya ulinzi wa amani vya UM na AU, katika juhudi zao za kuyatekeleza majukumu yaliopendekzwa na Baraza la Usalama. Pia ningelitaka kujua, mimi binafsi, masaibu yanayoukabili ule umma unaotegemea kupatiwa hifadhi na ulinzi kutoka wanajeshi wa kimataifa.”

KM Ban anatarajiwa kufanya mashauriano na viongozi wa Chad, Libya na Sudan kuhusu taratibu zinazofaa kuchukuliwa kipamoja, ili kuhakikisha vikosi vya mseto vya AU na UM - vitakavyojulikana kama vikosi vya UNAMID - vitaweza kupelekwa Darfur haraka iwezekanavyo kuendeleza operesheni zake, na pia kuhakikisha misaada ya kiutu na maendeleo, inayohitajika kupelekewa umma muhitaji, huwa inafikwisha kwa wakati na kwa urahisi na, vile vile, kuhakikisha mpango wa amani unaendelezwa kwa nidhamu ya kuridhisha.

Kwa mujibu wa KM Ban jumla ya wanajeshi 26,000 wa vikosi vya mseto vya UM na AU watapelekwa Darfur, kama ilivyopendekezwa na Baraza la Usalama mwezi Julai, wanajeshi ambao wataanzisha operesheni zao mapema mwakani.