Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa hapa na pale

Kwa hapa na pale

Mwakilishi wa UM huko DRC William Lacy Swing amelaani mauwaji ya mwanasiasa Floribert Chuy Bin Kositi, katibu wa jimbo wa chama cha RCD huko Goma, mji mkuu wa Kivu ya Kaskazini. Bw Swing anasema inaonekana kuna mtindo unaojitokeza ya kuwauwa viongozi wa kisiasa na biashara huko mashariki ya taifa hilo kubwa. Mkuu huyo wa MONUC ametoa mwito kwa wakuu wa DRC kuwatafuta na kuwahumu wahalifu wa kitendo hicho cha kikatili kinacho tokea wakati juhudi zina imarishwa kuleta amani katika eneo hilo.

Baraza la Usalama limekaribisha habari kwamba mazungumzo yanayo dhaminiwa na UM juu ya Sahara ya Magharibi kati ya Moroko na Chama cha Polisario pamoja na majirani zake, Algeria na Mauritania yamepangwa kuanza mwezi ujao. Mjumbe maalum wa KM kwa ajili ya Sahara ya Magharibi,Bw Peter van Walsum alilieleza baraza la usalama wiki hii kwamba pande zote zimekubaliana kuendelea na mazungumzo na kueleza hiyo ni hatua ya kwanza nzuri.

KM Bw Ban Ki-moon pamoja na mkuu wa shirika la mawasiliano ya kimataifa ya UM, ITU wameunga mkono mkutano wa viongozi baadae mwaka huu, wenye lengo la kuimarisha miundo mbinu ya teknolojia na habari na mawasiliano ya komputa barani Afrika ili kuendeleza maendeleo barani humo. Mkutano huo “Unganisha Afrika” utafanyika mjini Kigali hapo Oktoba 29 na 30 na unawakusanya pamoja wajumbe kutoka serekali, sekta za biashara na mashirika ya kimataifa kujaribu kutafuta njia kutanzua mwanya mkubwa wa mawasiliano ya komputa kote barani humo.