Tatizo la athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye miji

Tatizo la athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye miji

Ripoti ya Shirika la UM juu ya Makazi (UN-HABITAT) imeashiria ya kuwa katika mwaka 2007 tutashuhudia mabadiliko hakika kwenye tabia ya wanadamu, kwa ujumla, ambapo inaripotiwa fungu kubwa la umma wa kimataifa, utahajiri na kuukwepa utamaduni wa vijijini, kitendo ambacho kitawapatia umma huu utambulisho mpya na kujulikana kama viumbe vya miji, au kwa lugha ya KiLatina homo urbanus.

IN: Kwa kusema kweli sasa suala zima ambalo linajadiliwa sasa hivi hapa kama unavyojua ni jinsi maendeleo endelevu yanavoweza kuathirika kwa sababu ya ubadilikaji wa majira au hali ya hewa, na mimi kwa upande wangu nilikuwa nikitoa mada kuangalia suala hili kwa mtizamo wa miji na makazi, kwamba hali ya hewa ikiendelea kubadilika, kwa vyo vyote vile, mfumo wa makazi utabidi ubadilike, kwa sababu kama mito ikikauka inabidi wanavijiji wahame, wakitafuta maji. Majangwa yanavyozidi kusogea, wafugaji hawawezi tena kuendelea na kazi zao; kwa hivo wote wanasonga mijini. Na matatizo … nilizungumzia kwamba unakuta kwamba tuna wakimbizi wa kimazingira ndio wamejaa mijini. Utakuta kwamba …

AR:Unaweza kutufafanulia hawa wakimbizi wa mazingira ni nani hasa?

AT:Yaani hawa environmental refugees, au kweli wakimbizi wa mazingira ni watu ambao wanajikuta mijini kwa sababu wameshindwa; sio kwamba wanataka kuwa mijini, lakini hawawezi tena kuendelea kama wafugaji. Hawawezi tena kuendelea kama wakulima. Kwa hivyo sasa unakuta ndio – tayari wameingia kwenye vitongoji duni vya miji yetu hii na haya ni matatizo makubwa. Kwa hiyo mabadiliko ya hali ya hewa na majira yatabadilisha mfumo mzima wa makazi. Na utakuta kwamba mabadiliko yenyewe yanabidi yashughulikiwe kimakazi, kimiji. Kwa mfano sasa hivi kama kweli barafu zitaendelea kuyeyuka kama unavyojua kwamba kina cha maji kinaweza kikapanda na kama kikipanda miji mingi itazama. Na kama itazama unajua tena wenye nguvu ndio watapanda katika nyanja za juu, kwa hiyo unakuta kwamba masikini, watu makazi nyumba zitaharibika, kutakuwa kuna uharibifu mkubwa rasilmali. Kwa hiyo katika kujitayarisha hatuna budi kulenga makazi. Kwanza kuelewa kabisa kwamba makazi yataathirika – manake ndio binadamu anaishi katika makazi. Iwe vijiji, iwe miji midogo. Ziwe manispaa. Iwe miji mikubwa, ni hayo hayo … Na nakuja kusisitiza kwamba ni lazima tujiandae.

AR:Na mada hii italinganishwa na hichi kikao cha CSD ambacho kinaendelea … ?

AT:Sasa kikao, kama ulivyosema ndio kinaendeleza, na kikao hiki kina mlengo, kina tizama zaidi suala la nishati. Lakini hayo hayo kwa sababu sasa kama nyumba zikiharibika, utumiaji wa nishati wenyewe ndio umechangia katika kuharibu mazingira. Kwa sababu hizo carbon gas emissions zinatokana na, ni nishati -(AR: Umwagaji wa hewa chafu.) – ndio hiyo, ndio inaharibu, na ndio imetufikisha hapa tulipofika sasa hivi, kwa sababu hali ya hewa inazidi kuwa joto, wanavyosema wataalamu, nyuzi joto zinaongezeka. Kwa hivyo nishati, kwa hivyo suala hili sote hivi sasa tunaangalia kuna mambo mawili. Kwanza, lazima tuwe na nishati safi ambayo haichafui hali ya hewa yenyewe. Lakini sasa kufanya hivyo pia kunahitaji utaalamu, kunahitaji pesa; waekezaji – kwa sababu sasa hivi wanasayansi wameshagundua, wanaendelea kugundua, lakini sasa hivi haijafikia kuingiza katika kibiashara. Bei bado iko juu. Hata na hizo nguvu za jua, kwa mfano umeapisha .. kutumia nguvu za jua, hata na hiyo wind energy, nguvu za kutumia upepo, yote vipo lakini kwa kweli huwezi kusema kwamba vimeshaenea katika jamii. Bado viko katika nyanja za sayansi. Havijaingia kwenye ile commercial level, yaani kusema kwamba ni kitu ambacho unakwenda dukani, unataka kununua jiko la solar, mambo hayo bado yako katika hayajaenea. Kwa hiyo unakuta kwamba sasa watu ambao ni wa kima cha chini, masikini ndio kabisa hawawezi kupata vyombo hivi. Kwa hiyo unakuta kwamba, umaskini wenyewe unaendelea pia kuchangia katika kuendelea kuharibu, lakini pia mfumo wa maisha, katika miji yetu inabidi tubadilishe life style – mfumo wa maisha … Kila mtu anapenda awe gari lake. Lakini sasa unakuta kwamba kama huna miundo mbinu ya kutosha, hata kama barabara zipo, lakini unaendelea kuchafua hewa; sasa hiyo pollution, vitu ambavyo tunavizungumzia. Kwa hivyo utakuta wengine wanasema kwamba katika nchi zinazoendelea labda watu watumie baiskeli. Lakini haitoshi kutumia baiskeli. Kama watu wengine wanaendelea wenyewe kukaa mtu moja anakaa kwenye gari; kwa hivyo yote haya yanajadiliwa. Na mimi nayazungumzia kwa mtizamo wa makazi.

AR:Ndio nilikuwa nataka kufuatia kwa kuuliza vipi sera hizi, au mfumo huu mpya utaathiri zaidi mataifa yanayoendelea katika bara la Afrika, hususan katika Afrika Mashariki?

AT:Sasa, kama unavyofahamu, kwanza kuwaambia raia kwamba sasa watabidi watumie nishati, usafirishaji labda ambao hauchafui hali ya hewa. Unawaambia watu ambao wanashinda wanaangalia TV kwamba sasa wenyewe itabidi waende na baiskeli. Unajua kuna matatizo ya kiutawala pia! Na ndio maana inabidi nchi ambazo zinaendelea, kwanza unakuta zenyewe ndio bado hazijazipanga vizuri, yaani zenyewe ndizo zinashindwa kabisa utaratibu. Maanake sasa watu walikuwa wanasema, ‘jamani tuweke barabara, tuwe na gari.’ Leo unawaambia ‘ah, nyinyi mnatakiwa muwe na labda bicycle lanes.’ Kwa hivyo, ujengaji wa barabara hizi ambazo zitatunza mazingira pia, na [?] na gari zaidi. Kwa sababu huwezi tena kuwa na barabara nyembaba, lazima uwe na barabara ambayo pia ina vibarabara vyengine vya pembeni, kwa ajili ya watu ambao wanatembea kwa mguu, au watu wanaoendesha baiskeli, kusudi uwe na usalama. Kwa hivyo unakuta nchi zinazoendelea, na Afrika Mashiriki ikiwemo, ni kwamba zinahitaji pia kusaidiwa. Tunaziita adapatation, kwamba ni lazima tuwe na utaratibu, kwa jamii ya kimataifa, kusaidia hizi nchi kusudi ziweze nazo .. kujipanga. Lakini kitu ambacho nadhani sasa hivi kinakubalika kwa wote, ni kwamba hatuwezi kuendelea kama zamani – business as usual – yaani hiyo kwa kweli haitawezekana. Inabidi wote tukubali kubadilika. Lakini kubadilika sio kwa wale wanaoendelea; kubadilika pia ni kwa wale ambao wameshaendelea.

AR:Kwa hivyo sera za aina gani zinatakikana zitekelezwe kuhakikisha mataifa wanachama yanaweza kudhibiti vyema zaidi tatizo hili?

AT:Mimi nafikiria tukishakubaliana kwamba suala hili ni lazima lichangiwe, sasa wale ambao wamechafua mazingira ni zile nchi ambazo kwa kweli zimeendelea, zenyewe ndio chafuzi wa mazingira kuliko watu wote. Lakini sasa anayeathirika, anayeathirika sio yeye anaechafua. Tena utaona cha kusitikisha ni kwamba ile anaye haribu labda yeye ana miti yake, au makazi yake, yanaweza yakastahamili zaidi. Kama wana nyumba, nyumba madhubuti kama hapa mjini New York, kwa mfano, nyumba ni madhubuti, haziangushwi kwa upepo huu wa kawaida. Lakini au, kwa mfano, nchi. kama Japan – sasa hivi hata na tetemeko la ardhi sio tishio kwa nchi hiyo; kwa sababu yale majengo yamejengwa kitaalamu. Yanastahamili.

AR:Na wana uwezo wa kujenga majengo kama yale, lakini vipi katika mataifa yanayoendelea?

AT:Kabisa. Sasa wale ndio hawana. Kwa hivyo nasema kwamba, wanasema ngombe wa maskini hazai. Sasa tatizo ndio tunajikuta kwamba wale ambao hawajiwezi, ndio wanaathirika zaidi. Ukiangalia nchi za Afrika Mashariki, kwa mfano, Mlima wa Kilimanjaro ulikuwa kabisa umejaa theluji, ilikuwa ni kuvitio kikubwa sana kwa watalii kuja kuangalia barafu. Lakini inayeyuka, kwa kasi.

AR:Na inaathiri vile vile makazi chini kule kwa wale wote wanaotegemea maji yanayotoka milimani?

AT:Sasa si ndio hivyo. Kwa hivyo unakuta kwamba ile mito iliokuwepo haipo. Kwa hivyo sasa utakuta kwamba labda unaweza ukakuta kwamba wananchi wakazi wa pale, Wachaga, wanabidi wateremke sasa wakitaka kwenda kulima bondeni, manake sasa hivi migomba haipati maji ya kutosha. Kwa hivyo ndio na sasa watalii labda hawatakuja, manake sasa ule mlima haupendezi kama hauna theluji; kile kivutio kinaondoka. Kwa hivyo unakuta kwamba watu huku, katika nchi ambazo zimeendelea, Ulaya, Marekani na sehemu nyingine, wanatumia nishati mbaya, ambayo nishati ambayo ni chafu chafu, dunia inazidi, nyuzijoto zinapanda, Mlima wa Kilimanjaro unapoteza barafu anayelipa gharama za kuchafua mazingira yaliotoka mbali, unaweza kukuta ni mtu mwengine. Kwa hivyo ndio maana lazima suala hili lijadiliwe chini ya Umoja wa Mataifa, kwa sababu ni suala ambalo wana public good, ni kitu cha watu wote. Anayechafua sio ndiye lazima ndiye anayeathirika.

AR:Na katika kumaliza, una kauli yeyote ya mwisho ambayo itasaidia kuwafamisha wasikilizaji wetu juu ya umuhimu wa kulishughulikia suala hili hivi sasa kabla athari zake hazijaumiza umma wa kimataifa katika siku za mbele?

AT:Mimi nafikiria kwamba kwa labda wasikilizaji wanaweza tu kushauri kwamba, kwanza, kitu cha kwanza tuendelee kufuatilia mada hizi watu wanavyozungmza, mazungumzo haya kuyafuatilia kwa karibu, lakini kujiangalia sisi wenyewe pale tulipo, manake tusikate tamaa na kusema, kwanza, wanachafua kwengine mimi ninaathirika. Sisi wenyewe kila mtu, labda niseme hapa la Mwalimu Nyerere kwamba kila mtu atekeleze ule wajibu wake. Kwa hivyo katika .. pale ambapo mtu katika makazi yetu tulipo tuhakikishe kwamba miti haikatwi ovyo ovyo, kwamba tunajaribu na sisi kutumia nishati, nzuri, ambayo haichafui neighbourhood, pale tulipo. Tukianzia pale nadhani kujumuika kwa wote ndio kutaweza kusaidia suala hili.