Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii ya kimataifa yaadhimisha 'Siku ya Mazingira Duniani'

Jamii ya kimataifa yaadhimisha 'Siku ya Mazingira Duniani'

Tarehe 05 Juni huadhimishwa kila mwaka kuwa ni \'Siku ya Mazingira Duniani\'. Sherehe aina kwa aina hufanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa yaliopo New York na katika sehemu nyengine za ulimwengu ambapo UM huendeleza shughuli zake.~

KM wa UM Ban Ki-moon kwenye risala yake ya kuadhimisha ‘Siku ya Mazingira Duniani’ alieleza kuwa na wasiwasi juu ya kuongezeka kwa athari mbaya za mazingira ambazo huchochewa na hewa chafu inayomwagwa kwenye anga, kitendo ambacho, alionya, huharibu utulivu maumbile wa mazingira na hasa katika yale maeneo baridi ya ncha za dunia, kadhia ambayo inaashiria hatari ya kuzidi kwa kina cha bahari na kufumsha mafuriko ya kugharikisha mataifa kadha ulimwenguni.

Achim Steiner, mkuu wa Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) risala yake ilitilia mkazo ile hoja yenye kusisitiza kuwa udhibiti wa mazingira ya kimataifa ni kinga muhimu sana dhidi ya migogoro ya kimatabaka, kati ya watu masikini na watu matajiri, mizozo ambayo hufungamana na mabadiliko ya hali ya hewa, hasa ilivyokuwa makundi haya ya umma yote huwa yanagombania mali zile zile za asili, rasilmali ambazo, kwa bahati mbaya, bado zinaendelea kuadimika katika ulimwengu, kwa mfano ardhi zenye rutuba na maji safi.

Dktr Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) yeye alikumbusha ya kwamba sote tunahitajiwa kuimarisha, kwa nguvu moja huduma za afya ya jamii, kadhia ambayo ikitekelezwa kama inavyotakiwa, itasaidia pakubwa kuulinda umma wa kimataifa na athari zinazotokana na uchafuzi wa mazingira, hasa ilivyokuwa maafa ya mabadiliko ya hali ya hewa yanakadiriwa kusababisha vifo vya watu 60,000 kila mwaka duniani.

Mwanahabri wa Redio ya UM, Dianne Penn alipokuwa mjini Oslo, Norway majuzi alipata fursa ya kuonana na mwanaharakati wa kutunza mazingira wa Kenya, na pia mpokezi mashuhuri wa Tunzo ya Amani ya Nobel, Wangari Maathai. Dianne alimwomba Bi Wangari atume salamu maalumu kwa umma wa Afrika Mashariki kwa kuelezea umuhimu wa ‘Siku ya Mazingira Duniani’:

WM: “Nafurahi sana kutuma salaam za World Environment Day na kujulisha watu wote katika Afrika Mashariki hasa na Afrikaya Kati ya kwamba tunafurahia sana siku hii na ningetaka kuwakumbusha ya kwamba kitu ile ya muhimu kabisa ni

kulinda mazingira yetu na kitu kimoja ambayo kila mtu anaweza fanya ni kupanda mti na kuangalia miti ile ambayo inasimama bado. Na hasa kulinda misitu yetu katika Afrika Mashariki na Afrika ya Kati. Tuna misitu ya maana sana na mito yetu yote inatoka huko. Na tungetaka sote tuyachunge mazingira haya kwa sababu sisi na watakaotufwata watahitaji sana mazingira haya. Ahsanteni sana na kuweni na siku nzuri ya World Environment Day.”

Vile vile katika Makao Makuu ya UM kulifanyika shughuli mbalimbali kuiheshimu ‘Siku ya Mazingira Duniani’, ikijumuisha kampeni ya mbio za kupokezana, ilioandaliwa kwa kusudio la kuchangisha fedha za kuwasaidia watu milioni 20 ulimwenguni kupata maji safi itakapofika 2015. Miongoni mwa wakimbiaji walioshiriki kwenye kampeni hiyo alikuwemo mkimbiaji wa masafa marefu wa Kenya, Emmanuel Kibete ambaye,kwanza, alimuelezea mwandishi wa Redio ya UM, Israa Hamad juu ya namna mbio hizi zilivyotayarishwa:

EK: “Kwa sasa tutakuwa tunakimbia kupitia nchi 16 na ambayotutakuwa tunaeneza, tunajulisha watu kwamba wanahitaji kuwa na maji mazuri, tutakuwa tunachangisha pesa ya miradi mbalimbali ya maji kote duniani … Hii ni ndio kama relay,relay ya non-stop relay ambayo tunakuwa na vijiti, ama baton, ya kupitisha kwa mwengine. Unashika unaenda unampatia mwengine maasa ishirini na nne. So ni kama masaa 24 kwa siku saba. So hakuna kupumzika kwa muda wa siku 95, ninety five days.”

Sikiliza taarifa kamili kwenye idhaa ya mtandao.