Naibu KM aonya "Afrika imepwelewa kutekeleza MDGs"

Naibu KM aonya "Afrika imepwelewa kutekeleza MDGs"

Naibu KM Asha-Rose Migiro aliwasilisha ripoti mpya ya UM kuhusu maendeleo katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs)katika mataifa ya Afrika yaliopo kusini ya Sahara. Alionya ya kuwa juhudi za kuyakamilisha malengo hayo kwa wakati ziko nyuma na zinazorota.

Naibu KM alisema ni matumaini yake ripoti hii ya UM itawahamasisha walimwengu kuongeza juhudi zao katika kadhia muhimu zinazotakikana kuikamilisha miradi ya kupunguza umasikini, kwa utaratibu unaowajibika kisheria na wenye uwazi, na kutambua kwamba wakati umewadia wa kuacha tabia ya kubishana kanuni za kimsingi juu ya masuala yanayohusu MDGs na wanahitajiwa kuyatekeleza Malengo ya MDGs kidharura na kwa vitendo.

Halkadhalika, Naibu KM aliyataka mataifa wanachama wa Kundi la G-8 yaliokutana karibuni kwenye Mkutano Mkuu uliofanyika Ujerumani kuitumia fursa ya mkusanyiko wao wa wafadhili wa kimataifa, kuandaa ratiba halisi ya kuongeza misaada ya maendeleo kwa kila taifa muhitaji katika bara la Afrika kuanzia sasa hadi 2015, mwaka ambao jamii ya kimataifa ilidhamiria kukamilisha Malengo ya MDGs na kupunguza, angalau kwa nusu, hali ya umasikini na ufukara katika nchi zinazoendelea.