Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Juni 14 iliadhimishwa na UM kuwa ni Siku ya Kuchangia Damu Duniani, na mwaka huu Shirika la Afya Duniani (WHO) limetilia mkazo ulazima wa mama wazazi kupatiwa damu salama, hasa ilivyokuwa kila mwaka inakadiriwa mama wajawazito nusu milioni ziada hufariki kwa sababu ya kuvuja damu kunakokithiri wakati wa mimba na wakati wa kujifungua.~

Mashirika ya UM yanayohudumia umma wa Kifalastina kwenye Maeneo Yaliokaliwa Kimabavu ya Wafalastina (OPT) yamewasilisha taarifa yenye kuelezea "wasiwasi mkubwa" walionao juu ya kukithiri kwa vurugu na mapigano katika eneo la Tarafa ya Ghaza, hali ambayo tangu tarehe 09 Juni imesababisha makumi kadha ya vifo na majeruhi, ikjumuisha pia vifo vya watumishi wawili wa UM. Ripoti imesema UM umekerwa zaidi na taarifa zilizonesha kufanyika mashambulio dhidi ya mahospitali, magari ya wagonjwa na mauaji ya kihorera, nje ya taratibu za mahkama.

Mjumbe Mkuu wa UM juu ya Ushirikiano wa Tamaduni za Kimataifa, Raisi wa zamani wa Ureno, Jorge Sampaio majuzi aliwaambia waandishi habari hapa Makao Makuu, baada ya mkutano wa mashauriano na KM Ban Ki-moon, ya kwamba katika miaka miwili ijayo tume anayoiongoza inajitayarisha kuandaa miradi ya kuboresha uhusiano, mafahamiano na maelewano miongoni mwa tamaduni zinazotofautiana kwa kutumia ilimu, vyombo vya habari, vijana na huduma za uhamaji, kadhia ambazo anaamini zitasaidia kuondosha mfarakano uliojiri sasa hivi na ambao umegawanyisha tamaduni za Mataifa ya Magharibi na Uislamu.