Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwimbaji Stara Thomas wa Tanzania kutetea uzazi salama

Mwimbaji Stara Thomas wa Tanzania kutetea uzazi salama

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Kudhibiti Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) imetangaza ya kuwa mwimbaji wa Tanzania, Stara Thomas, aliye maarufu katika ulimwengu unaozungumza Kiswahili, atatumia ujuzi wake wa kisanii kwa kushirikiana na UM katika huduma za kusaidia mama waja wazito nchini kwao na katika bara la Afrika kujikinga dhidi ya vifo vya katika uzazi na vifo vya watoto wachanga.

Katika Tanzania, imeripotiwa kutukia vifo vya mama wazazi 578 katika kila uzazi wa watoto 100,000. Zaidi ya nusu ya mama waja wazito katika taifa hilo hujifungua majumbani bila ya kupata msaada wa wakunga wajuzi.

Mutribu Stara amesema ni matumaini yake nyimbo zake zitasaidia kuihamasisha Serekali ya Tanzania kuongeza idadi ya wakunga na pia kuboresha kijamii afya ya uzazi.