Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suala la Usomali lazingatiwa tena na Baraza la Usalama

Suala la Usomali lazingatiwa tena na Baraza la Usalama

Baraza la Usalama lilikutana kwenye kikao cha faragha tarehe 14 Juni kusailia hali, kwa ujumla, katika Usomali na pia kusikiliza ripoti ya Lynn Pascoe, Makamu KM juu ya Masuala ya Kisiasa juu ya matukio ya ziara yake ya Usomali hivi majuzi ambapo pia alitembelea nchi jirani zinazopakana na taifa hilo la Pembe ya Afrika.

Baada ya mkutano wa Baraza la Usalama Pascoe alikabiliana na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu ambao aliwaambia ya kwamba ni muhimu sana sasa hivi, kwa jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kunapatikana mafanikio ya kuridhisha kwenye ule Mkutano wa Upatanishi wa Taifa, hali ambayo huenda ikaipatia raia wa Usomali fursa imara ya kurudisha tena utulivu na amani nchini mwao, hasa baada ya vurugu na mtafaruku kuselelea kwenye eneo lao kwa muda wa miaka kumi ziada mfululizo. Kadhalika, Baraza la Usalama limetoa taarifa rasmi inayoashiria kuwa inatayarisha mradi wa kuanzisha operesheni mpya za kimataifa za ulinzi wa amani katika Usomali.