Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Tarehe 26 Juni huadhimishwa kuwa ni Siku ya Kimataifa dhidi ya Mateso, na kwenye risala ya KM Ban Ki-moon kuiheshimu siku hii walimwengu walikumbushwa wajibu wao katika kuwapatia tiba inayofaa waathiriwa wote wa mateso, kote duniani; na KM vile vile aliyahimiza Mataifa Wanachama kuuridhia haraka Mkataba wa Kimataifa dhidi ya Mateso.~

•Ripoti ya Ofisi ya UM ya Kudhibiti Vitendo vya Uhalifu na Madawa ya Kulevya (UNODC) imethibitisha ya kuwa katika mwaka 2007 imeonekana waliopewa mamlaka ya kutekeleza sheria kimataifa wamewania kukabiliana na biashara haramu ya madawa ya kulevya duniani, na pia katika matumizi ya madawa haya, kwa mwelekeo wa kutia moyo uliohakikisha jinai hiyo haitokithiri kimataifa.

•Shirika la wahamiaji la UNHCR limearifu kwamba wahamiaji wa KiFalastina 1,400 waliokimbia Baghdad hivi sasa wamekwama kwenye hali mbaya sana ya maisha kwenye zile kambi za mipakani kati ya Iraq na Syria, na wanahitajia kufadhiliwa na jamii ya kimataifa misaada ya dharura ya kihali ili kunusuru maisha.

•Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetangaza kuingiza kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia maeneo matatu mapya yaliopo katika mataifa ya Bukini, Uchina na Jamhuri ya Korea, uamuzi ambao umejumuisha maeneo ya kutunzwa maumbile 833.

•Kadhalika kwa mara ya kwanza katika historia ya UNESCO shirika limewajibika kufuta kutoka Orodha ya Urithi wa Dunia eneo liliopo Oman ambalo hutumiwa kutunza aina ya Choroa Adimu wa Kiarabu, kwa sababu Serekali imeamua kutenga asilimia 90 ya eneo hilo kusaka petroli.

•Ripoti mpya ya Chuo Kikuu cha UM imehadharisha kwamba tatizo la kuenea kwa jangwa – ikishinikizwa na mabadiliko karaha ya hali ya hewa – ni mchanganyiko hatari sana wenye kuashiria utata zaidi dhidi ya utulivu wa kimataifa.

•Mjumbe wa UM juu ya Maendeleo ya Visiwa Vidogo Vidogo na Mataifa Masikini ya LDCs, Anwarul Chowdhury aliwaambia waandishi habari hapa Makao Makuu kwamba kunatakikana juhudi za kimataifa za haraka kuyasaidia maeneo masikini kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na marekibisho ya kimaumbile yenye uwezo wa kugharikisha na kuyaangamiza milele maeneo haya.