Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani

Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani

Tarehe 03 Mei huadhimishwa kila mwaka na jamii ya kimataifa kuwa ni ‘Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani’. Ujumbe wa risala ya KM Ban Ki-moon kuiheshimu siku hii, mwaka huu, ulitilia mkazo umuhimu wa kuzingatia, na kutafuta suluhu ya kuridhisha, inayotakikana kuwakinga waandishi habari dhidi ya taathira mbaya wanazokumbana nazo katika kutekeleza kazi zao.

Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kwa upande wake, liliiadhimisha ‘Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari’ kwa kuandaa mkutano wa maalumu siku mbili katika mji wa Medellin, Colombia uliojadilia na kusailia mada muhimu inayohusu uhuru wa kueleza ukweli, bila kukhofu pingamizi za kutoka kwa wenye madaraka.

Miongoni mwa taadhima nyenginezo zilizoandaliwa na jumuiya ya kimataifa katika Makao Makuu kuiheshimu ‘Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari’ iliambatana na mjadala maalumu ulioandaliwa na Idara ya DPI, uliojumuisha wataalamu mbalimbali wa fani ya vyombo vya mawasiliano ya habari, ambao walibadilishana mawazo juu ya muktadha usemao "Tufanye Nini Ziada Kuboresha Uhusiano kati ya UM na Uhuru wa Vyombo vya Habari?"