Skip to main content

Mkuu wa DPI anaripoti sera mpya mbele ya COI

Mkuu wa DPI anaripoti sera mpya mbele ya COI

Makamu-KM Kiyotaka Akasaka, mkuu mpya wa Idara ya Habari kwa Umma ya UM (DPI) aliwakilisha sera mpya ya taasisi yake mbele ya wajumbe wa kimataifa waliohudhuria kikao cha ufunguzi cha Kamati ya Habari, au Kamati ya COI. Alisema sera na ratiba mpya ya kazi na shughuli za DPI, chini ya uongozi wake, zitayapa umuhimu, na umbele zaidi masuala manne yanayohusu huduma za usalama na amani ya kimataifa, mabadiliko ya hali ya hewa, maendeleo ya kiuchumi na jamii, na utekelezaji wa haki za binadamu.~

Bw Akasaka aliiambia Kamati ya COI ya kuwa atahakikisha mabadiliko yote yalioandaliwa na DPI yatatekelezwa kwa utaratibu na utulivu usiochafua nidhamu za kazi ziliopo sasa. Alitilia mkazo, pia, kwamba licha ya dhamira ya kuwakilisha sera mpya DPI “imefanikiwa kukamilisha malengo yake, taratibu taratibu” kwa sababu ya kujitayarisha mapema zaidi kukabiliana na mageuzi haya. Alikumbusha Akasaka kwamba ripoti za DPI huwa zinapewa usikivu mkubwa, wa kuaminika, na mashirika ya habari kadha wa kadha ya kimataifa. Alitoa mfano wa Mkutano wa Kiwango cha Juu wa 2006 wa Baraza Kuu la UM juu ya Suala la Uhamaji. Alisema katika kikao hiki, asilimia 90 ya ripoti zote za vyombo vya habari vya kimataifa zilizungumzia taarifa zilizotayarishwa na na kuandaliwa na Idara ya DPI, kuhusu jukumu muhimu la UM katika kudhibiti bora tatizo la uhamaji duniani.

Kadhalika, Makamu KM wa Idara ya Habari kwa Umma alieleza kwamba watu milioni 50, kila mwaka, wamesajiliwa kuzuru mtandao wa UM. Vile vile alibainisha watu milioni 300 ziada hupata fursa ya kusikiliza vipindi vya Redio ya UM, na kukumbusha asilimia kubwa ya vipindi hivyo vinaweza kusikilizwa kwenye kompyuta, kwa kupitia idhaa ya mtandao.

Kuhusu shughuli za Vituo vya Habari vya UM (UNIC), viliopo katika sehemu mbalimbali za dunia, Akasaka alifahamisha ya kuwa ndizo taasisi zenye kutusaidia kueneza na kufahamisha, “kwa lafdhi, na sauti za kienyeji, na pia kwa karibu zaidi, umuhimu wa shughuli za UM” kwenye maeneo yao, pindi zitatumia uwezo wao kama inavyostahiki.