Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaonya uchafuzi wa hewa ya majumbani unakandamiza afya

WHO yaonya uchafuzi wa hewa ya majumbani unakandamiza afya

Shirika la Afya Duniani (WHO) limewasilisha ripoti inayosema asilimia 5 ya jumla ya vifo vinavyotukia ulimwenguni sasa hivi, kwenye mataifa 21 yanayoendelea, husababishwa na nishati ngumu inayotumiwa kwa kupikia na kueneza joto ndani ya majumba. Kwa mujibu wa WHO, matumizi ya nishati ngumu – kama vile makaa, kuni, vinyesi na mabaki ya mimea – ni moja ya matishio makubwa 10 yanayohatarisha afya ya jamii kijumla.

UM umeyanasihi mataifa husika kuanza kutumia nishati ngumu mbadala, zilizo madhubuti na safi, mathalan, mafuta ya kerosini au gesi ziliyoyeyushwa za petroli, matumizi ambayo yakiendelezwa yatasaidia pakubwa kukomesha hatari kwa afya ya umma katika mataifa 11 na, baadaye, kuwakinga vifo vya mapema, kila mwaka, watu bilioni moja na nusu (1.5).

UM umesisitiza kwamba ni jukumu letu sisi sote kuhakikisha umma muathiriwa, hususan watoto wadogo na wanawake, huwa wanapatiwa huduma za kihali za kuboresha afya, kwa ujumla, badala ya kuwapa madhuru.