-- Juhudi za kuboresha biashara ya maji ya madafu kwa kutumia teknolojia ya kisasa -- Pendekezo la kudhibiti biashara ya silaha ndogo ndogo ulimwenguni

-- Juhudi za kuboresha biashara ya maji ya madafu kwa kutumia teknolojia ya kisasa -- Pendekezo la kudhibiti biashara ya silaha ndogo ndogo ulimwenguni

Watu wenye kuishi kwenye maeneo ya joto, na karibu na minazi – au wale wenye uwezo wa kununua madafu kutoka wachuuzi wa kwenye miji - hutambua vyema kwamba maji ya madafu ni kinywaji kinachoburudisha sana, chenye natija kwa afya na pia kina ladha tamu kabisa.

Lakini licha ya sifa hizo, na licha ya kuwa maji ya madafu yana uwezo wa kuleta faida kubwa za kiuchumi, pindi yatauzwa kwenye soko la dunia la vinywaji vya chupa au mikebe, nchi zinazoendelea hazikufanikiwa kuuza maji ya madafu yenye ladha asilia kwenye soko zao au kwenye soko za kimataifa. Kwa nini? Kwa sababu mara tu baada ya madafu kukatwa, hewa yenye kuchanganyika na ujoto joto, husababisha maji hayo kuanza kuchacha, na hupoteza, kwa kasi, ile ladha nzuri pamoja na umbo lake asilia. Watu wa biashara ya vinywaji duniani waliojaribu kuuza maji ya madafu ya chupa, waliepukana na tatizo hilo pamoja na hatari ya kuchipuka vijidudu vyenye madhara, kwa kutumia mtambo wa halijoto ya daraja ya juu kabisa kupasha moto maji ya madafu. Lakini utaratibu huu uliharibu ladha asilia ya maji ya madafu na kuangamiza virutubisho vya afya viliomo ndani ya kinywaji hicho.

Hivi karibuni, kulipatikana mafanikio ya kutia moyo katika teknolojiya ya kuhifadhi ladha asilia ya maji ya madafu, maendeleo ambayo yaliripotiwa na Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO). Shirika la FAO lilielezea juu ya kubuniwa utaratibu mpya unaotumia teknolojiya yenye uwezo wa kutunza maji ya madafu kwa muda mrefu zaidi na kuyakinga na tatizo la kuchacha, na vile vile kuibakisha ladha asilia ya maji ya madafu baada ya kuyatia ndani ya chupa au mkebe. Utaratibu huu hujulikana kama ‘utunzaji baridi’ na umekusudiwa kuyasaidia makampuni, pamoja na wakulima wadogo wadogo, hususan wale wakulima waliopo katika nchi zinazoendelea, kupata uwezo wa kuuza maji ya madafu ya chupa yanayobakiliza ladha asilia na virutubisho maumbile vya afya. Kwa mujibu wa FAO, utaratibu huu wa ‘utunzaji baridi’ hauna gharama kuu, na wala hauhitajii kisomo kikubwa. Ni utaratibu unaoweza kutumiwa na hata wale wenzetu walio wachuuzi wa mitaani.

Mpango wa ‘utunzaji baridi’ unaopendekezwa na Shirika la FAO una uwezo wa kubakiza ladha tamu asilia ya maji ya madafu ya kuuzwa kwenye chupa. FAO imechapisha kijitabu cha mafunzo, cha kuwaongoza wafanyabiashara na wakulima wadogo wadogo wa mataifa yanayoendelea, namnaya kutumia kwa urahisi zaidi mradi wa ‘utunzaji baridi’ wa maji ya madafu.

Teknolojiya hii ya ‘utunzaji baridi’ ilibuniwa na kutathminiwa katika kisiwa cha Jamaika, kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha West Indies, pamoja na Bodi la Viwanda vya Nazi na Taasisi ya Utafiti wa Kisayansi ya Jamaika.

Ripoti ya pili kwenye makala hii inahusika na pendekezo la kudhibiti athari za silaha ndogo ndogo duniani.

Majuzi, wanadiplomasiya wa kimataifa wa vyeo vya juu katika UM, akiwemo Kamishna Mkuu Mstaafu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Mary Robinson, na vile vile wawakilishi wa vikundi maarufu vya jamii za kiraia, walijumuika kwenye Makao Makuu kwa mazungumzo na wanahabari, na kuanzisha kampeni ya kuitika mwito wa KM Ban Ki-moon wa kuzihimiza Serekali za Mataifa Wanachama kumtumia maoni yao juu ya “uwezekano wa kutayarisha mswada” wa mkataba mpya wa kudhibiti biashara ya kuhamisha, kuuza na kununua silaha ndogo ndogo ulimwenguni. KM Ban aliyataka Mataifa Wanachama yote kumtumia jawabu zao kabla ya Aprili 30 mwaka huu.

Miongoni mwa wanadiplomasiya waliohudhuria kikao na waandishi habari, kuanzisha kampeni ya kuhimiza nchi wanachama kubuni mkataba wa kudhibiti biashara ya silaha alikuwemo Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kenya katika UM, Balozi Zachary Muburi-Muita. Baada ya kikao na waandishi habari Redio ya UM ilimhoji Balozi Muita.

Kwa mahojiano kamili sikiliza idhaa ya mtandao.