Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu lafanya mapitio ya udhibiti wa UKIMWI duniani

Baraza Kuu lafanya mapitio ya udhibiti wa UKIMWI duniani

Mapema wiki hii Baraza Kuu la UM lilifanyisha kikao maalumu, cha mapitio, kuhusu maendeleo kwenye juhudi za kukithirisha uwezo wa kuwapatia umma wa kimataifa uangalizi bora, misaada ya afya, matibabu na hifadhi inayotakikana dhidi ya virusi vya UKIMWI (VVU).

Kikao kinakutana mwaka mmoja baada ya Mataifa Wanachama yalipoahidi kuimarisha mchango wao ziada katika kupiga vita janga la UKIMWI na kudhibiti hatari inayoletwa na VVU. Ahadi hizi zilijumuishwa kwenye Mwito wa Azimio la Kupambana na VVU/UKIMWI liliopitishwa na Baraza Kuu mwaka jana.

Risala ya KM Ban Ki-moon mbele ya kikao cha Baraza Kuu ilithibitisha tena kwamba UM na mashirika yake, pote ulimwenguni, yataendelea kujitahidi, kwa nguvu moja, kukidhia mahitaji yote ya kupiga vita UKIMWI hivi sasa na kipindi cha muda mrefu ujao.

Raisi wa Baraza Kuu la UM, Sheikha Haya Rashed Al Khalifa, yeye kwenye hotuba yake ya ufunguzi, alikumbusha ya kuwa juhudi za kudhibiti janga la UKIMWI ni harakati za kushindana na wakati. Kwa hivyo, aliwahimiza viongozi wa dunia kujaribu kuharakisha mchango wao katika kuzitekeleza ahadi walizotoa mwaka jana, kama inavyopaswa.

Vile vile mwanaharakati, na pia mtungaji sera za maendeleo wa kutoka Botswana, Elizabeth Mataka ameteuliwa rasmi na Ban Ki-moon kuwa Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afrika juu ya UKIMWI.