Mijadala ya mwaka ya CSW inazingatia haki za wanawake na mabinti

5 Aprili 2007

Kamisheni ya Baraza Kuu juu ya Haki za Wanawake, au Kamisheni ya CSW, kabla ya kukamilisha kikao cha mwaka, kwa 2007, ilipitisha mswada wenye mapendekezo manne muhimu: awali, jumuiya ya kimataifa ilitakiwa kuwatekelezea wanawake wa Kifalastina haki halali za kimsingi; pili, watoto wa kike walitakiwa wapatiwe hifadhi bora dhidi ya VVU/UKIMWI; tatu, tabia ya kutahiri mabinti ikomeshwe, na mwishowe, kuhakikisha mila ya kuoza watoto wa kike wenye umri mdogo inasitishwa. Mapendekezo haya manne yanalingana na kiini cha mijadala ya kikao cha 51 cha Kamisheni ya CSW.

Ajenda ya mwaka huu ya mijadala ya Kamisheni ya CSW ilitilia mkazo umuhimu wa kuandaa taratibu za kimataifa, ili kukomesha vitendo karaha vya unyanyasaji na matumizi ya nguvu na mabavu dhidi ya mabinti na wanawake.

Kamisheni ya CSW ilibuniwa na Baraza la UM juu ya Maendeleo ya Kiuchumi na Jamii (ECOSOC) kwa lengo la kuandaa sera za kimataifa zitakazoimarisha maendeleo ya wanawake na kuleta usawa wa kijinsia duniani. Kamisheni hiyo ina wajumbe 45, na kila mjumbe huchaguliwa na Baraza la Maendeleo ya Kiuchumi na Jamii (ECOSOC), na huwakilisha taifa moja mwanachama.

Kikao cha mwaka 2007 kilihudhuriwa na maelfu ya wajumbe waliowakilisha serekali wanachama, pamoja na jumuiya za kiraia, asilimia kubwa yao ikiwa wanawake na mabinti walioshiriki kwenye matukio mbalimbali yaliofanyika kwenye Makao Makuu ya UM, na pia walihudhuria mijadala na mikutano iliosailia taratibu za kuharakisha utekelezaji wa haki za kijinsia duniani.

Mchango wa wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yasio ya kiserekali, yaani mashirika ya NGOs, katika kuandaa sera za kuimarisha haki za kijinsia ulimwenguni, ni kitendo kinachothaminiwa sana na UM na taasisi zake, kwa ujumla. Bi Amina Zuberi ni mjumbe aliohudhuria vikao vya Kamisheni ya CSW na aliwakilisha mashirika mawili ya NGOs kutoka Kenya. Tulibahatika kufanya mazungumzo na Bi Amina kwenye studio za idhaa ya Redio ya UM, ambapo alitupatia maoni ya mashirika yasio ya kiserekali juu ya mijadala ya mwaka huu ya kikao cha 51 cha Kamisheni ya CSW.

Tafadhali sikiliza mahojiano kamili kwenye idhaa ya mtandao.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter