Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo ya uchumi Afrika yameegamia msingi dhaifu: ECA

Maendeleo ya uchumi Afrika yameegamia msingi dhaifu: ECA

Mnamo mwanzo wa wiki, Ejeviome Eloho Otobo, ofisa mchumi wa UM, aliyewahi kufanya kazi na Kamisheni ya UM juu ya Maendeleo ya Uchumi kwa Afrika (ECA), iliopo Addis Ababa, Ethiopia aliwakilisha mbele ya waandishi habari wa kimataifa kwenye Makao Makuu ripoti yenye muktadha usemao \'Taarifa juu ya Hali ya Uchumi Afrika 2007\'. Alisema uchumi wa Afrika, kwa ujumla, uliendelea kukuwa kwa asilimia tano mnamo miaka mitatu iliopita, lakini mwelekeo huo uliselelea kwenye msingi dhaifu sana.~

Moja ya tabia ya uchumi wa bara la Afrika ni kuwa unategemea sana biashara ya kuuza bidhaa za msingi katika soko la kimataifa, bidhaa ambazo katika kipindi cha miezi kumi hadi kumi na nane iliopita, zilifaidika sana na kujiri muongezeko wa ghafla wa bei katika soko hilo, hususan bei za mafuta ya petroli na mali nyengine za asili.

Alionya Otobo kwamba sera ya kutegemea mapato, kutokana na biashara iliolemewa na bei za kigeugeu katika soko la kimataifa, ni utaratibu unaohatarisha na kudhoofisha maendeleo ya kiuchumi wa bara la Afrika. Alisisitiza ya kuwa mataifa ya Kiafrika yanawajibika, kwa kulingana na wakati, kuleta mageuzi ya sera za uchumi wao, na ni lazima kwayo yapanue na kufanya anuwai ya harakati za kiuchumi ili kuepukana na athari zinazowasilishwa na miporomoko ya bei za bidhaa ya mali asili katika soko la kimataifa.