Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jumuiya ya kimataifa yasikitika na kulaani mashambulio ya mabomu Algeria na Iraq

Jumuiya ya kimataifa yasikitika na kulaani mashambulio ya mabomu Algeria na Iraq

Maofisa wa UM wa vyeo vya juu, wakijumuika na KM Ban Ki-moon walishtumu na kulaani vikali mashambulio maututi yaliotukia majuzi kwenye Bunge la Iraq, Baghdad, ambapo Wabunge kadha walifariki na wingi wengineo kujeruhiwa.

Baada ya msiba huo KM Ban aliwanasihi viongozi wote wa Iraq washirikiane kipamoja kwenye juhudi za kukomesha, halan, vitendo vya matumizi ya nguvu na vurugu, kwa matarajio hatua hiyo itafanikiwa kuwarudishia hali ya utulivu na amani nchini mwao.

Vile vile, KM Ban alilaani vikali mashambulio ya mabomu ya kigaidi yaliofanyika kwenye mji wa Algiers, Algeria karibuni, tukio ambalo lilisababisha vifo kadha vya raia wasio hatia, na pia kujeruhi idadi kubwa ya watu, mashambulio ambayo tuliarifiwa yalikusudiwa hasa kumdhuru Waziri Mkuu wa Algeria, Abdelaziz Belkhadem. KM Ban aliwatumia Serekali na umma wa Algeria mkono wa taazia, hususan aila za waathiriwa wa tukio hilo. Kwa mujibu wa nasaha alioitoa KM Ban, vitendo vya kigaidi vilivyoshadidi karibuni kwenye jimbo la Maghreb, yaani eneo la Afrika Kaskazini, vinahitajia mchango jumuiya, kwa jamii ya kimataifa kufanikiwa kuukomesha ugaidi unaokandamiza na kuchafua utulivu wa maisha ya kawaida kwa umma kijumla.