Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vurugu la Usomali limefurutu ada, na ni la hatari mno

Vurugu la Usomali limefurutu ada, na ni la hatari mno

Ijumanne, Makamu KM juu ya Misaada ya Dharura, John Holmes aliripoti mbele ya Baraza la Usalama kwamba hali ya mapigano nchini Usomali kwa sasa ni mbaya sana, hususan kwenye mji wa Mogadishu. Holmes aliirudia tena taarifa hii pale alipokutana na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu:~

Holmes alisema kutokana na ukosefu wa usalama pamoja na ushirikiano dhaifu na wale wenye kuendesha Serekali ya Mpito, huduma za UM pamoja na zile za mashirika yasio ya kiserekali zimepwelewa, na wafanyakazi wanaohudumia misaada ya kiutu wameshindwa kuwafikia raia muhitaji wanaokimbia mapigano, na kushindwa hata kuzifikia zile ghala zinapowekwa misaada ya dharura, ya kihali, inayotakiwa kupatiwa umma muathiriwa. Kadhalika, mashirika yanayotoa misaada yamenyimwa ruhusa ya kwenda kwenye viwanja vya ndege vya K50 na Merka, karibu na mji wa Mogadishu, na misaada ya kihali ya kimataifa, kwa sasa, imefanikiwa kuwafikia watu waliong’olewa makwao 60,000 tu, wingi wao wakiwa wanawake, watoto wadogo na watu wazee.

Kwa mujibu wa Holmes, tangu mapigano kufumka kati ya vikosi vya Serekali na makundi ya wapinzani, mnamo tarehe mosi Februari, raia 321,000 (laki tatu na elfu ishirini na moja) waliuhajiri mji wa Mogadishu. Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imeripoti ya kwamba mnamo miezi mitatu ya kwanza ya 2007, majeruhi 1,000 walipokewa kwenye hospitali mbili kuu za Mogadishu, idadi hiyo ikijumuisha, vile vile, majeruhi 200 ziada waliopokelewa katika mwisho wa wiki iliopita. Holmes alisema KM Ban Ki-moon yeye anaendelea kujitahidi kuyahimiza makundi yanayohasimiana Usomali, kuwacha mapigano na, wakati huo huo, Baraza la Usalama, kwa upande wake, linajaribu kuharakisha uwezekano wa kuongeza wanajeshi 6,000 wa ulinzi wa amani kutoka Umoja wa Afrika (AU), na kusaidia wanajeshi 1,000 wa Uganda waliopo sasa hivi nchini Usomali.