Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Kufyeka Malaria Afrika

Siku ya Kufyeka Malaria Afrika

Wiki hii, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kurudisha Nyuma Malaria imewasilisha mradi mpya wa kufadhilia huduma za kupiga vita maradhi ya malaria Afrika. Jumuiya hiyo inatumai kwamba nusu ya maombi yote ya yale mataifa yanayohitajia msaada huo yatatekelezewa mataifa husika, hususan katika bara la Afrika, eneo ambalo, kila mwaka, asilimia 90 ya vifo milioni 1 vya malaria hutukia.

Ushirikiano baina ya mashirika ya UM kuhusu afya (WHO), maendeleo ya watoto (UNICEF), miradi ya Maendeleo (UNDP) na Benki Kuu ya Dunia, pamoja na serekali kadha husika, na vile vile wabia wengineo, ikijumuisha mashirika wahisani ya kimataifa na taasisi za kitaaluma mbalimbali, umewania kuimarisha kampeni ya kupunguza vifo vya malaria, kwa watoto wachanga, angalau kwa nusu, itakapofika 2010. Misaada inayoambatana na juhudi hizi imeshafanikiwa kuwapatia watoto wachanga, katika maeneo kadha husika, dawa kinga na pia vile vyandarua vilivyonyunyiziwa dawa dhidi ya mbu, kadhia ambazo, kwa ujumla, zimesaidia pakubwa kwenye udhibiti bora wa malaria kwenye maeneo hayo. Mathalan, takwimu za UM zimethibitisha ya kwamba katika kipindi cha miaka miwili baada ya kupokea misaada ya kupiga vita malaria katika mataifa ya Msumbiji, Rwanda na Zanzibar (Unguja) idadi ya vifo vya watoto wachanga iliteremka kwa kiwango kikubwa, baina ya asilimia 40 mpaka 90.

Mfuko wa Kimataifa wa Kupiga Vita UKIMWI, TB na Malaria ni taasisi ya kimataifa inayoshirikisha sekta binafsi na ya kiraia, na ni taasisi yenye kuungwa mkono na UM. Mnamo miaka sita iliopota taasisi hii ilifanikiwa kufadhilia jumla ya dola bilioni 2.6 zilizotumiwa kuhudumia miradi mbalimbali ya kudhibiti vifo vya watoto wachanga dhidi ya malaria duniani.