Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makundi yote DRC yaharamisha haki za kibinadamu, imeripoti UM

Makundi yote DRC yaharamisha haki za kibinadamu, imeripoti UM

Ofisi ya UM juu ya Haki za Kibinadamu ya Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (MONUC) WIKI HII imetoa ripoti maalumu kuhusu namna haki za kimsingi zinavyotekelezewa raia kwa ujumla.

Ripoti ilibainisha ya kwamba vitendo vya kushutusha vilithibitika kufanyika dhidi ya raia wasio hatia, vitendo ambavyo vilikiuka maadili ya kiutu. Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa (UM) uligundua raia kuuliwa kihorera, wengine hutekwa nyara na kutoroshwa kwa mabavu, na mara nyengine hukumbwa na ukamataji wa jumla, na raia pia huteswa na kutendewa maovu, halkadhalika, kwa sababu ya uhusiano wao wa kisiasa. Vile vile imeoenkana raia wengine huwa wanaingiliwa na kunajisiwa kwa mabavu kwa sababu wanafuata chama fulani. Utafiti wa UM ulishughulikia utekelezaji wa haki za kibinadamu katika DRC kwa kipindi kilichojumlisha miezi ya Juni hadi Disemba 2006.

Ripoti ya MONUC ilisema makundi yote yalishiriki katika ukiukaji huo wa haki za kibinadamu, yakijumuisha majeshi ya taifa (FARDC), Shirika la Upelelezi (ANR), walinzi wa Jamhuri (RG) na Polisi wa Taifa wa Kongo (PNC) pamoja na walinzi wa Jean-Pierre Bemba, mgombea uraisi aliyeshindwa na vile vile makundi ya Wahutu wa Rwanda.

MONUC imearifu kwamba kunahitajika, hatua kali kuchukuliwa haraka katika DRC ili kukomesha tabia ya kuendeleza jinai kwa kiburi cha kutokhofu adhabu.