Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sikukuu ya Wanawake wa Kimataifa

Sikukuu ya Wanawake wa Kimataifa

Tarehe 08 Machi kila mwaka huadhimishwa na walimwengu kuwa ni Sikukuu ya Wanawake wa Kimataifa. Hapa kwenye Makao Makuu ya UM, mjini New York, kulifanyika taadhima mbalimbali za kuiheshimu siku hiyo, zikijumuisha mikutano, warsha za wataalamu na tafrija aina kwa aina.

Mada ya mwaka huu iliangaza kwenye zile juhudi za dharura, zinazotakikana kukomesha vitendo karaha vya unyanyasaji na utumiaji wa mabavu dhidi ya wanawake na watoto wa kike.

Kwenye kikao maalumu kilichodhaminiwa na mashirika ya UM, kilichofanyika Alkhamisi, tarehe 08 Machi (2007) kwenye Makao Makuu kuiheshimu ‘Sikukuu ya Wanawake wa Kimataifa’, KM wa UM, Ban Ki-moon alitoa risala yenye kuonya ya kwamba “unyanyasaji na utumiaji mabavu dhidi ya akina mama na watoto wa kike, ni vitendo vya dhulma vilivyokakamaa na kuselelea, takriban katika tamaduni zote, na katika kila nchi za bara zote za ulimwengu.”

Baraza la Usalama lilikutana na kutoa taarifa maalumu ya Raisi wa Baraza iliyosisitiza mchango muhimu wa wanawake katika kusuluhisha na kujikinga na migogoro.

Kamishna Mkuu kwa Haki za Kibinadamu, Louise Arbour, akirudia tamko la KM Ban, alikumbusha kwenye risala yake ya kuwa vitendo vya kutumia nguvu dhidi ya wanawake ni jinai ya kijinsiya, iliyoenea sasa hivi kote ulimwenguni, na alishtumu ni mara chache sana makosa haya hupatiwa adhabu mahakamani; mathalan, alisema, ushahidi wa taasisi za UM umethibitisha kwamba ni chini ya asilimia 5 tu ya washitakiwa wa vitendo karaha vya uingiliaji wa mabavu, au ubakaji, hupatikana na hatia wanapofikishwa mahakamani. Kadhalika, alisema watoto wa kike na wanawake milioni 130, ambao bado wangali hai, wamelazimishwa kutahiriwa kwa nguvu, kwa kisingizio cha ati walitekelezewa mila za kijadi.

Kwa kulingana na bayana hiyo ndipo KM Ban, alipoamua kwenye risala yake ya kuadhimisha ‘Sikukuu ya Wanawake wa Kimataifa’ kupendekeza kwa Serekali zote za nchi wanachama, pamoja na mashirika ya kimataifa, jumuiya za kiraia na vile vile sekta binafsi, kuchangisha juhudi zao kwenye viwango vyote vya kijamii, ili wafanikiwe kuwasilisha mageuzi yenye natija sawa za kijinsiya, na kuboresha maisha ya umma wa kiume na kike, kote duniani.