Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya Watu Duniani kuongezeka kwa bilioni 2.5 mwaka 2050

Idadi ya Watu Duniani kuongezeka kwa bilioni 2.5 mwaka 2050

Mapema wiki hii, bibi Hania Zlotnik, Mkurugenzi wa Idara ya UM juu ya Udhibiti wa Muongezeko wa Idadi ya Watu Duniani alizungumza na waandishi habari kwenye Makao Makuu, na kuwasilisha ripoti mpya yenye matokeo ya utafiti kuhusu viashirio vya viwango vya uzazi duniani kwa miaka ijayo.

Kwa mujibu wa bi Zlotnik, utafiti wa Idara yake unaashiria kwamba itakapotimu mwaka 2050, idadi ya umma wa kimataifa itaongezeka kutoka jumla tulionayo sasa ya watu bilioni 6.7 na kufikia watu bilioni 9.2, ikjumlisha muongezeko wa watu bilioni 2.5. Muongezeko huu, ripoti ilisema, unalingana na kipimo cha idadi ya watu waliokuwepo duniani katika mwaka 1950.

Kadhalika, Idara ya Udhibiti wa Idadi ya Watu inaashiria jumla ya watu wazee katika 2050 itaongezeka kwa bilioni 1, yaani wale watu waliozidi umri wa miaka 60, hasa katika mataifa yanayoendelea. Utafiti huu wa UM umethibitisha ya kuwa idadi ya watu itaendelea kuzeeka kwa kasi, halkadhalika, katika mataifa mengi ulimwenguni, kwa sababu ya kuporomoka kwa viwango vya uzazi; na kwa sababu asilimia kubwa ya umma wa kimataifa katika karne tuliomo sasa hivi huwa inaishi kwa muda mrefu zaidi. Bayana hii humaanisha mataifa yatawajibika kukuza uekezaji unaoofaa, katika huduma za uangalizi na utunzaji wa wazee, pamoja na kwenye huduma za kuimarisha ilimu.

Viashirio vya takwimu za UM juu ya muongezeko wa idadi ya watu duniani, kuweza kuthibitishwa kihakika, vitategemea mafanikio yatakayopatikana katika juhudi za kimataifa katika kudhibiti maambukizo ya maradhi ya UKIMWI duniani, na pia kwenye zile huduma za tiba ya kurefusha maisha kwa wagonjwa waliopatwa na virusi vya UKIMWI.