Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Wakati KM Ban Ki-moon alipokuwa kwenye ziara ya Mashariki ya Kati mapema wiki hii, alichukua fursa hiyo na kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Riyadh, Saudi Arabia, ambapo kwenye risala yake alitoa mwito wa kuhimiza viongozi wanachama wajitahidi kufanya kila wawezalo kuutekeleza ule Mpango wa Amani juu ya tatizo la Falastina na Israili, pamoja na kuwataka waongeze bidii zao vile vile katika kuipatia suluhu mizozo husika mengineyo katika Darfur, Sudan, Usomali na vile vile ile mizozo iliojiri katika Lebanon na Iraq. ~

Martin Scheinin, Mkariri maalumu wa Baraza la Haki za Kibinadamu anayehusika na hifadhi ya haki za msingi kwenye harakati za kupiga vita ugaidi, katika ripoti aliowakilisha mjini Geneva wiki hii alishtumu ya kuwa sera ya, baadhi ya mataifa, ya kutumia vitambulisho vya asili ya utaifa wa mtu, dini au ukabila kutahadharisha au kuthibitisha hatari ya ugaidi, ni sera isio sahihi na inakiuka haki za kimsingi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) na Jumuiya ya Mashirika ya UM dhidi ya UKIMWI (UNAIDS), yamethibitisha kihakika ya kuwa kitendo cha kutahiri wanaume ni moja ya njia ziada inayoweza kutumiwa kusaidia umma wa kimataifa kupunguza, kwa asilimia sitini, ile hatari ya kuambukizwa na virusi vya UKIMWI.

WHO imeripoti ya kuwa ina matumaini ya kutia moyo yenye kuashiria kwamba pindi bidii za kumudu tiba dhidi ya maradhi ya minyoo itahimiliwa kwa kiwango kinachoendelezwa kwa sasa hivi kwenye mataifa husika, walimwengu tutaweza kuyafyeka maradhi haya duniani kote katika mwaka 2009.