Skip to main content

Katibu Mkuu Ban Ki-moon ameanza kazi na kuteua maofisa wapya wa ngazi za juu, akiwemo Naibu KM

Katibu Mkuu Ban Ki-moon ameanza kazi na kuteua maofisa wapya wa ngazi za juu, akiwemo Naibu KM

Januari 01, 2007 Ban Ki-moon, aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Nchi za Kigeni wa Jamhuri ya Korea au Korea ya Kusini, alianza kazi rasmi kama ni KM wa nane wa Umoja wa Mataifa.

KM Ban aliahidi kuyatekeleza mahitaji ya walimwengu kwa kumuisha michango ilio imara kutoka jamii ya kimataifa. Alisema atayapa umuhimu masuala yanayohusu vurugu la Darfur (Sudan), mizozo ya Mashariki ya Kati, na pia Lebanon, Iran, Iraq, Korea ya Kaskazini na vile vile masuala yanayohusu hifadhi na ulinzi unaotakikana kuimarisha haki za kiutu duniani, pamoja na taratibu zinazofaa kuihamasisha jumuiya ya kimataifa kuongeza bidii zao ili tufanikiwe kuyafikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwa wakati kabla ya 2015.

KM Ban alionana na watumishi wa UM waliopo Makao Makuu pamoja na wenziwao waliopo katika ofisi nyengine zilizosambaa sehemu mbalimbali za dunia, kwa kutumia njia ya mawasiliano ya vidio, na alibadilishana nao mawazo na fikra juu ya ushirikano unaohitajika kuimarisha vizuri zaidi na kuboresha kazi zitakazozaa natija kwa masilahi ya umma wa kimataifa.

Kadhalika KM Ban Ki-moon wiki hii aliteua maofisa watano wapya wasaidizi, miongoni mwao akiwemo mwenzetu, Michele Montas wa kutoka Haiti, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Kifaransa ya Redio ya UM na ambaye hivi sasa atachukua nafasi ya Msemaji rasmi wa KM. Vijay Nambiar, mwanadiplomasiya wa India aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kuendesha Ofisi ya KM Ban. Hali kadhalika,Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dktr Asha-Rose Migiro aliteuliwa Ijumaa kuwa Naibu KM mpya wa Umoja Mataifa.