Baraza la Usalama lapendekeza kuchukuliwe hatua za dharura katika Jamhuri ya Afrika ya Kati

19 Januari 2007

Raisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Januari, Balozi Vitaly Churkin wa Shirikisho la Urusi aliwaambia waandishi habari waliopo Makao Makuu ya UM kwamba wajumbe wa mataifa 15 katika Baraza hilo walikubaliana kupendekeza kwa KM Ban Ki-moon atayarishe haraka tume ya utangulizi itakayozuru Chad na pia Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa mashauriano na serekali za mataifa haya mawili. Baadaye KM alitakiwa atayarishe ripoti ya mapema itakaousaidia UM kuandaa operesheni za ulinzi wa amani katika eneo lao.

Baraza la Usalama lilichukua uamuzi wa kupeleka tume ya utangulizi katika Chad na pia Jamhuri ya Afrika Kati baada ya kupatiwa taarifa juu ya hali ilivyo, kwa ujumla, kwenye maeneo hayo, na Mjumbe wa KM kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jenerali Lamine Cisse na Mshauri wa Misaada ya Kiutu kwa taifa hilo, Toby Lanzer. Tume ya utangulizi inatazamiwa kuondoka New York kuelekea kwenye maeneo husika mwisho wa wiki.

Ripoti ya KM juu ya ziara hiyo itakamilishwa na kuwasilishwa mwezi Februari, na inatazamiwa kuratibu mapendekezo juu ya namna operesheni za ulinzi wa amani zitakavyoendeshwa kwenye maeneo hayo, kwa taratibu zitakazonufaisha umma muathiriwa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud