Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za Umoja wa Mataifa katika kufufua utulivu na amani Usomali

Huduma za Umoja wa Mataifa katika kufufua utulivu na amani Usomali

Mapema wiki hii UM ulipeleka tume maalumu ya ukaguzi, kwenye mji wa Mogadishu, Usomali kwa mara ya kwanza tangu Serekali ya Mpito kuchukua madaraka. Dhamira ya ujumbe huo ni kutathminia mahitaji ya misaada ya kiutu kwa raia wa Usomali.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Kiutu (OCHA) imeripoti ya kwamba hatua iliochukuliwa na Serekali ya Kenya ya kufunga mipaka yake na Usomali hivi karibuni, na kuzuzia wahamiaji kuingia nchini, ni tukio liliozusha matatizo ya afya kwa raia wa Kisomali walionaswa mipakani, ambao baadhi yao insemekana walibanwa na kuambukizwa na magonjwa ya kuharisha na pia malaria. Kwa upande mqwengine Shirika la Afya Duniani (WHO)limefanikiwa kuhudumia madawa, nishati na vifaa vya tiba zile hospitali ziliopo Usomali ya kusini.

Mshauri Mkaazi wa UM juu ya Misaada ya Kiutu kwa Usomali, Eric Laroche ameinasihi jamii ya wafadhili wa kimataifa kujinyakulia fursa iliyodhihiri karibuni Usomali kufufua tena huduma zao za kupeleka misaada ya kiutu kwa raia muhitaji.

Alkhamisi Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Francois Lonseny Fall alizuru Mogadishu kwa mashauriano na Raisi Abdullahi Yusuf, pamoja na kukutana na wawakilishi wa jumuiya za kiraia ambao walizingatia taratibu za kuchukuliwa kipamoja kukabiliana na masuala yanayohusu upatanishi kati ya makundi yanayohasimiana, na uwezekano wa kurudisha tena usalama na amani ya taifa. Fall aliihimiza Serekali ya Mpito ya Usomali kuchukua fursa iliyojitokeza sasa hivi nchini kuanzisha shughuli za utawala katika wilaya zote, na majimbo yote ya taifa. Wakati huo huo Fall alipendekeza kwa Serekali kuhakikisha viongozi wa makundi ya wanamgambo hawatorudishiwa tena madaraka waliojinyakulia siku za nyuma.