Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapitio ya Mkutano wa UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa Ulimwenguni

Mapitio ya Mkutano wa UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa Ulimwenguni

Kuhusu ripoti nyengine zinazoambatana za Mkutano wa Nairobi, Yvo de Boer, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya UM ya Mfumo wa Mkataba juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa Ulimwenguni (UNFCCC) alinakiliwa akisema aliridhika na mafanikio yaliopatikana kwenye Mkutano wa UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa Ulimwenguni.

Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) nalo kwa upande wake vile vile limewasilisha ripoti ya utafiti unaoashiria itakapofika mwaka 2040 tutashuhudia muongezeko mkubwa wa dhoruba, tufani, ukame na mafuriko yatakayochochewa na mabadiliko ya hali ya hewa, na kukadiria hasara itakayoletwa na maafa hayo kukiuka mabilioni kwa mabilioni ya madola. Ripoti ya UNEP imependekeza kubuniwe bima mpya, zitakazoshirikisha sekta za kiraia na za binafsi, kuyasaidia mataifa yanayoendelea kudhibiti uharibifu unaoashiriwa kwenye maeneo yao kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Risala ya KM Kofi Annan mbele ya wajumbe wa kimataifa iliwashtumu wale wote ambao bado wanaendelea kukanusha kuwepo hatari inayozushwa na mabadiliko ya hali ya hewa, hatari ambayo huathiri afya ya wanadamu, huduma za kuazalisha chakula, na pia kuathiri maisha ya zile jamii zinazoishi kwenye maeneo yanayokabiliwa na kunyanyuka kwa kina cha bahari, na hata kuhatarisha usalama na amani ya kimataifa. Alikumbusha KM ya kuwa wakanushaji wa bayana hiyo “hawana hoja za kusikilizwa, wamepitwa na wakati na mawazo yao yamekosa dira ya kuwadhihirishia ukweli wa mambo ulivyo.”