Eritrea yashtumiwa kuharamisha mapatano ya kusitisha mapigano mipakani

20 Oktoba 2006

KM Kofi Annan akijumuika na Baraza la Usalama wiki hii wametoa taarifa ya pamoja kuishtumu Eritrea kwa kupeleka vifaru 15 na pia wanajeshi karibu 1,500 kwenye lile Eneo la Muda la Usalama (TSZ) liliopo mipakani na Ethiopia.

Majeshi ya taifa ya Eritrea, yaani majeshi ya EDF, yaliripotiwa kuteka nyara kituo cha ukaguzi cha Shirika la Ulinzi wa Amani la UM la UNMEE liliopo kwenye eneo linalojulikana kama Sekta ya Magharibi. UM umethibitisha kitendo hiki kinatengua Maafikiano ya 2000 ya Kusitisha Uhasama kati ya Eritrea na Ethiopia na kina mwelekeo unaobashiria kupalilia hali ya hatari katika siku za usoni. Serekali ya Eritrea imenasihiwa na jamii ya kimataifa kuondosha, halan, majeshi yake kutoka Eneo la TSZ mipakani na kutakiwa ishirikiane haraka na UM ili kurudisha amani na utaratibu wa kusitisha mapigano na kulihifadhi eneo na hatari ya kuzuka tena mapigano ambayo athari yake italeta vurugu na machafuko katika eneo zima la Pembe ya Afrika.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud