Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumbukumbu ya ziara ya Makamu KM juu ya Masuala ya Kiutu katika Afrika

Kumbukumbu ya ziara ya Makamu KM juu ya Masuala ya Kiutu katika Afrika

Mapema wiki hii Jan Egeland, Makamu KM Juu ya Misaada ya Kiutu ya Dharura alikutana na waandishi habari mjini Nairobi, Kenya baada ya kukhitimisha safari ya siku nane kwenye maeneo matatu yaliokabiliwa na matatizo ya kiutu barani Afrika; yaani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (JKK), Uganda na Sudan ya Kusini.

Egeland aliwaambia waandishi habari kwamba kwa nadharia yake yeye binafsi anaamini hali katika JKK na katika eneo la Uganda ya kaskazini imechangisha msiba adhimu wa kiutu kwa vizazi vya karne yetu ya sasa. Lakini licha ya mazingira hayo Egeland alibashiria hali, kwa ujumla, katika miezi ya karibuni inaelekea kurejesha utulivu wa amani, ambapo pia anatarajia mamia elfu ya wale raia waliongolewa mastakimu yao watafanikiwa fursa ya kurejea makwao.

Kadhalika, Egeland alisema ana matumaini baadhi ya maelfu ya wale watoto pamoja na wanawake waliotekwa nyara katika siku za nyuma na kundi la LRA wataachiwa huru na waasi hawo. UM unakisia watoto karibu 20,000 vile vile walinyakuliwa na LRA, kundi ambalo liliripotiwa pia kuwakata viungo na kulemaza makorja ya raia kadha wa kadha wasio hatia katika Uganda, na hata kunajisi kwa kashfa kuu makumi elfu ziada ya wanawake.