Katibu Mkuu ahudhuria kikao cha wahisani wa kimataifa kwa Darfur mjini Brussels.

Katibu Mkuu ahudhuria kikao cha wahisani wa kimataifa kwa Darfur mjini Brussels.

KM Kofi Annan wiki hii alihudhuria kikao maalumu cha wahisani wa kimataifa waliokusanyika katika mji wa Brussels, Ubelgiji kuzingatia uwezekano wa kuchangia msaada maridhawa kufadhilia operesheni za amani za AMIS, yaani vikosi vya ulinzi wa amani vya Umoja wa Afrika (AU) katika Darfur, Sudan.

Katika hotuba ya ufunguzi kwenye mkutano ulioandaliwa kuzingatia mpango wa kuboresha operesheni za amani za AU katika Darfur, KM Kofi Annan alisema matokeo ya mkusanyiko huo muhimu “yanategemewa kuimarisha zaidi maisha ya maelfu ya watoto, pamoja na raia wa kike na kiume katika Darfur.”

KM alisema jamii ya kimataifa, hivi sasa, imejaaliwa upenu unaowakilisha fursa adhimu ya kuukomesha mgogoro katili wa Darfur kwa haraka. Aliahidi ya kuwa “UM hauna njama zo zote za siri za kulinyakua eneo hilo” la Sudan.

Alitilia mkazo kwenye risala yake kwamba “lengo hasa la UM kwa Darfur ni kuhakikisha umma unaoteseka katika eneo hilo unakidhiwa mahitaji yao ya dharura ya kiutu.” Zaidi ya jukumu la kufadhilia operesheni za vikosi vya AU msaada wa kuimarisha kazi zake, kimantiki, alihoji KM, ni dhahiri jumuiya ya kimataifa vile vile itawajibika, hatimaye, kupeleka katika Darfur vikosi vya ulinzi wa amani vya UM kuwa kama “wasaidizi wa kurudisha utulivu wa amani na hifadhi inayotakikana ya raia, na sio, kama inavyodhaniwa, kuwa wavamizi wenye dhamira ya kulikalia mabavu eneo hilo.”

Kwa maelezo kamili sikiliza taarifa.