Virusi vya Corona kama dharura ya afya ya umma:Taarifa za UN News Kiswahili
Mlipuko uliripotiwa mara ya kwanza Wuhan China Desemba 31, 2019

Ukurasa huu unaleta pamoja taarifa kuhusu muongozo kutoka kwa Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO na Umoja wa Mataifa kuhusu mlipuko wa sasa wa virusi vya corona au COVID-19, ambavyo viliripotiwa mara ya kwanza Wuhan, China mnamo Desemba 31, 2019. Tafadhali tembelea ukurasa huu kupata taarifa za kila siku. WHO inafanya kazi kwa karibu na wataalam wa kimataifa, serikali na wadau kupanua ujuzi wa kisayansi kuhusu virusi hivi vipya, kutokana na jinsi vinavyosambaa na athari zake  na kutoa ushauri kwa nchi na watu, kuhusu hatua za kuchukua kwa ajili ya kulinda afya na kuzuia kuenea kwa mlipuko.

Virusi vya COVID-19 sio hatari kama vilivyo virusi vingine vya aina hiyo-WHO

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema inaonekana kwamba virusi vya corona COVID-19 sio hatari kama vilivyo virusi vingine vya aina hiyo ikiwemo vile vinavyosababisha homa ya mafua, SARS au virusi vya corona vinavyosababisha matatizo ya kupumua MERS na kuongeza kwamba asilimia 80 ya wagonjwa wana viwango vya chini vya  virusi na watapona.