Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kinachoendelea Libya chaweza kuwa uhalifu wa kivita, 47 wauawa na 181 kujeruhiwa siku tatu zilizopita:UN

Watoto ni kundi lililoko hatarini zaidi katika migogoro.
UN OCHA/GILES CLARKE
Watoto ni kundi lililoko hatarini zaidi katika migogoro.

Kinachoendelea Libya chaweza kuwa uhalifu wa kivita, 47 wauawa na 181 kujeruhiwa siku tatu zilizopita:UN

Amani na Usalama

Katika siku tatu zilizopita watu 47 wameuawa na wengine 181 kujeruhiwa katika machafuko yanayoendelea mjini Tripoli Libya na viunga vyake huku ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ikitoa onyo kuwa mashambulizi hayo dhidi ya raia na miundombinu yao yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO miongoni mwa waliouawa tisa ni raia wakiwemo madaktari wawili ambao wamekuwa wakitoa huduma muhimu kwa raia wanayoihitaji mjini Tripoli, huku mmoja wa madaktari ameripotiwa kuuawa wakati akiwa katika huduma za dharura kwenye gari la kubebea wagonjwa. WHO inasema imeorodhesha zaidi ya mashambulizi 46 ambayo yameathiri wahudumu wa afya na vituo vya afya kote nchini Libya kwa mwaka 2018-2019 mashambulizi ambayo yamekatili maisha ya wahudumu wa afya na wagonjwa wanane na kujeruhi wengine 24. WHO imeongeza kuwa, “hali tete inayoendelea, makombora yanarovurumishwa kila uchao na mapigano vinatishia maisha ya raia na kuwa kikwazo kikubwa kwa wahudumu wa masuala ya kibinadamu. Na kuendelea kwa mashafuko hayo Libya mamia ya vituo vya afya vimefungwa na zaidi ya hospital 20 zimeharibiwa au kufungwa.”

Kinachoendelea nchini Libya

Kwa upande wake kamishina Mkuu wa haki za binadamu Michelle Bachelet leo amezikumbusha pande zote katika mzozo wa Libya kuhusu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa kuhakikisha kwamba raia na miundombinu yao wanalindwa , akiwataka kuchukua hatua ili kuhakikisha raia hawabebi tena gharama za vita hivyo. Kupitia taarifa yake iliyosomwa na msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Ravina Shamdasani mjini Geneva amesema kuna haja ya hatua za haraka za kuwalinda wasiojiweza wakiwemo wakimbizi na wahamiaji huku akionya kwamba mashambulizi dhidi ya raia huenda yakawa ni uhalifu wa vita na kwamba “watu wa Libya kwa muda mrefu wamejikuta katikati ya pande zinazokinzana na kukabiliwa na madhila makubwa ikiwemo ukiukwaji wa haki za binadamu.”

Bachelet amesisitiza kwamba misingi ya kutofautisha , kujizuia na kuchukua tahadhari ni lazima iheshimiwe kila wakati kwani “kuwalenga raia kwa makusudi au miundombinu ya raia kunaweza kuwa ni uhalifu wa vita.” Pia ametoa wito kwa serikali kuhakikisha jela na mahabusu hazitelekezwi na kwa pande zote kuhakikisha kwamba mahabusu wanatendewa haki kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Nini kifanyike

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mashambulizi yanayoendelea mjini Tripoli na viunga vyake ikiwemo shambulio la anga lililofanywa Jumatatu na jeshi la serikali ya Libya (LNA) dhidi ya uwanja wa ndege wa Mitiga.

Katibu mkuu ametoa wito wa kusitisha mara moja operesheni zote za kijeshi ili kutuliza hali na kuzuia machafuko hayo kuwa vita kubwa. Amesisitiza kwamba katika mgogoro wa Libya hakuna suluhu ya kijeshi na kuzitaka pande zote kujihusisha katika majadiliano mara moja ili kufikia suluhu ya kisiasa na kusema mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya yuko tayari kuwezesha mazungumzo hayo. Ameongeza kuwa Walibya wote wanastahili amani, usalama, ustawi bora na kuheshiwa kwa haki za binadamu.