Habari Mpya

Makamanda waasi katika Ituri, DRC wahamishwa Kinshasa na UM

Shirika la Ulinzi wa Amani la UM katika JKK (MONUC) limeripoti kufanikiwa kuwahamishia kwenye mji wa Kinshasa wale makamanda 16 waliokuwa wakiongoza makundi ya waasi katika eneo la Ituri. Kitendo hiki, ilisema MONUC, ni hatua kubwa katika kurudisha utulivu wa kijamii na kuimarisha amani kwenye jimbo la uhasama la kaskazini-mashariki ya nchi.

Ongezeko la harakati za kijeshi mipakani Ethiopia/Eritrea kutia wasiwasi jamii ya kimataifa

Ripoti ya karibuni ya KM wa UM kuhusu hali mipakani kati ya Ethiopia na Eritrea, yaani kwenye ile sehemu ya Pembe ya Afrika ijulikanayo kama Eneo la Usalama wa Muda (TSZ), imeonekana kuwa ni ya wasiwasi mkubwa.

IFAD kusaidia wanavijiji masikini Lesotho

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Kimataifa kwa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) limeanzisha mradi mpya wa dola milioni 8.7 kusaidia wanavijiji masikini 37,000 katika Lesotho. Mradi huu utawafadhilia wanavijiji husika mchango wa fedha za kuekeza kilimo chenye natija kiuchumi na kijamii kwenye maeneo yao.

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon ameihimiza Pakistan kuwatoa vizuizini wafungwa wote wapinzani waliotiwa ndani majuzi, akiwemo pia Asma Jahangir, mtaalamu anayehusika na haki za uhuru wa kidini na kiitikadi; na pia KM alipendekeza kwa wenye madaraka Pakistan kuchukua hatua za haraka kurudisha tena utawala halali wa kidemokrasia nchini.

Msanii wa Tanzania ashirikiana na UNFPA kuhudumia uzazi bora

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Udhibiti wa Muongezeko wa Watu Duniani (UNFPA)Thoraya Obaid alikumbusha kwenye risala yake ya karibuni kwamba umma wa kimataifa umeingia kwenye karne ambayo hawatovumilia tena vifo vya mama wakati wa kuzaa. Alisema UNFPA itajitahidi kufanya kila iwezalo, kwa ushirikiano na nchi husika, kuhakikisha janga hili linakomeshwa kote duniani.

Fafanuzi za Mpatanishi wa AU kwa Darfur juu ya Mkutano wa Sirte

Mazungumzo ya upatanishi kuhusu mgogoro wa Darfur, yaliofanyika kwenye mji wa Sirte, Libya kuanzia Oktoba 27 (2007) na kuongozwa na Mjumbe Maalumu wa KM kwa Darfur Jan Eliasson pamoja na Dktr Salim Ahmed Salim aliye Mpatanishi wa Umoja wa Afrika (AU) kwa Darfur, yamekamilisha awamu ya kwanza ya majadiliano kwa matumaini ya kuwa wadau wote watakutana tena baada ya wiki chache kusailia awamu ya pili juu ya taratibu za marekibisho zinazofaa kuchukuliwa kipamoja ili kurudisha utulivu na amani Sudan magharibi.

Kamati ya CTC yasailia udhibiti wa ugaidi

Kamati ya Baraza la Usalama dhidi ya Ugaidi au Kamati ya CTC ilipohitimisha mijadala ya siku tatu kwenye Makao ya UM mjini Nairobi Kenya, ilitoa taarifa ya pamoja na pia mpango wa utendaji, uliowakilisha karibu darzeni tatu ya mashirika ya kikanda na kimataifa, maafikiano ambayo yalilenga juhudi za kuimarisha uwezo wa nchi zao kuwanyima magaidi fursa ya kuvuka mipaka kihorera.

Vikosi vya UNAMID vyaanzisha operesheni mpya Darfur

Vikosi vya mseto vya UM/UA kulinda amani katika Darfur, yaani vikosi vya UNAMID vilianzisha rasmi operesheni zake katika jimbo hilo la Sudan Magharibi mnamo mwisho wa Oktoba. Operesheni hizo zinaambatana na ufunguzi wa Makao Makuu ya UNAMID kwenye mji wa El Fashir.

Baraza la Usalama laongeza muda wa UNMIS kuimarisha amani Sudan

Baraza la Usalama limepitisha azimio la kuongeza kwa miezi sita zaidi operesheni za kulinda amani za UNMIS. Shirika la UNMIS ni taasisi ya UM inayosimamia kusitishwa mapigano ya miaka 21 kati ya Sudan kusini na kaskazini.

Asilimia kubwa ya watoto walionyakuliwa Chad wanaishi na wazee

Mashirika ya UM, ikijumuisha lile shirika linalohusika na mfuko wa maendeleo ya watoto, UNICEF na lile linalosimamia huduma za wahamiaji, UNHCR yakichanganyika na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC yameripoti kwa kauli moja ya kuwa wale watoto 103 waliotuhumiwa kuibiwa hivi karibuni nchini Chad, kwa madai walikuwa ni watoto mayatima wanaohitaji familia za kuwatizama kihali na mali imebainika kihakika, baada ya uchunguzi kufanyika na wahudumia misaada ya kiutu kwamba kati ya idadi hiyo watoto 91 walikuwa na wazee wao halali na sio mayatima abadan. Watoto 12 waliosailia sasa hivi wanaendelea kufanyiwa uchunguzi ziada kutafutiwa wazee wao na kuthibitisha kama ni mayatima au la.