Habari Mpya

Ripoti ya UNEP yahusisha mabadiliko ya hali ya hewa na mifumko ya vurugu Sudan

Fafanuzi za utafiti wa Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) zimethibitisha ya kwamba hakuna dalili Sudan itafanikiwa kudumisha usalama na amani katika nchi bila ya kudhibiti kidharura uharibifu wa kasi wa mazingira.

WFP inaiomba Kenya kuruhusu misaada ya chakula Usomali

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (WFP) limetoa mwito maalumu unaoisihi Serekali ya Kenya kuruhusu malori 140 yaliokodiwa na UM na yaliochukua shehena za chakula, kuvuka mpaka wa kaskazini-mashariki na kuingia Usomali.

Watuhumiwa watatu wa makosa ya vita Sierra Leone kupatikana na hatia ya mashtaka 11

Mahakama Maalumu juu ya Jinai ya Vita Sierra Leone imetoa hukumu yake ya kwanza wiki hii ambapo watuhumiwa watatu wa Jeshi la Baraza la Mapinduzi – yaani Alex Tamba Brima, Brima Bazzy Kamara na Santigie Borbor Kanu - walipatikana na hatia ya mashtaka 11 yanayohusikana na makosa ya vita na vile vile jinai dhidi ya utu. Hukumu juu ya adhabu ya watuhumiwa hawa itatolewa na Mahakama kati ya mwezi Julai.

NKM atahudhuria Mkutano Mkuu wa AU Ghana

Naibu KM (NKM) Asha-Rose Migiro anatazamiwa kuelekea Afrika na Ulaya mwisho wa wiki. NKM atamwakilisha KM kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Afrika (AU) utakaofanyika mwanzo wa Julai mjini Accra, Ghana. Kabla ya hapo NKM Migiro ataelekea Vienna, Austria kutoa hutuba ya ufunguzi kwenye \'Jopo la 7 la Dunia la Uvumbuzi Mpya Ziada wa Shughuli za Serikali\'. Baada ya hapo ataelekea Guinea-Bissau, ikiwa ziara ya kwanza rasmi ya KM au NKM tangu taifa hilo kujiunga na UM.

Baraza la Usalama lataka kuanzishwe tume ya kuchunguza vikwazo dhidi ya Charles Taylor

Baraza la Usalama limepitisha kwa kauli moja azimio linalomtaka KM Ban Ki-moon kuanzisha tume maalumu ya wataalamu wa shughuli za fedha na biashara ya almasi, watakaopewa madaraka ya kuchunguza “madai yanayoaminika” dhidi ya Raisi wa zamani wa Liberia Charles Taylor, madai yenye kusisitiza kuwa Taylor bado ana uwezo na fursa ya kutumia kuhodhi mali nyingi sana ambayo imeekewa vikwazo na Baraza la Usalama mwaka 2004, licha ya kuwa Taylor sasa hivi yumo kizuizini.

Hapa na Pale

William Clay, Mtaalamu wa UM juu ya lishe bora wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) ameripoti kwamba kumethibitishwa mabibi au nyanya, ni fungu la umma wa kimataifa muhimu linalojumuisha rasilmali kubwa ya kutumiwa mara kwa mara katika huduma za maendeleo, hasa katika ulezi na udhibiti wa lishe bora kwa watoto, na katika utunzaji wa afya ya jamii.~

Sudan yakubali vikosi vya mseto vya kimataifa kwa Darfur

Baada ya kufanyika mashauriano ya kiufundi, ya siku mbili, kwenye mji wa Addis Ababa, Ethiopia katika wiki hii, kati ya wawakilishi wa UM na wale wa kutoka AU, pamoja na wajumbe wa Serekali ya Sudan, kulidhihirika fafanuzi za kuridhisha juu ya yale masuala yaliokuwa yakikwamisha utekelezaji wa mpango wa kupeleka vikosi vya mseto kulinda amani katika jimbo la magharibi la Darfur. Baada ya kikao cha Addis Ababa kulitolewa taarifa ya pamoja kati ya Serekali ya Sudan na AU iliosema ya kuwa Sudan imeridhia na kuidhinisha ule mpango wa kupeleka vikosi vya mseto vya UM na AU kwenye jimbo la Darfur.

Biashara za vijijini Afrika zitafaidika na mfuko mpya wa UM

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) lilitangaza majuzi mjini Cape Town, Afrika Kusini kwenye mkutano wa Athari za Uchumi wa Dunia kwa Afrika, ya kwamba litaanzisha taasisi mpya ya mfuko wa maendeleo kusaidia wanavijiji masikini katika Afrika, kupata fedha za kuanzisha aina mpya ya biashara kwenye maeneo yao.

Umoja wa Mataifa kumkumbuka KM wa zamani Kurt Weldheim

Alkhamisi, tarehe 14 Juni UM ulipokea taarifa ya kuhuzunisha kuhusu kifo cha aliyekuwa KM wa nne wa UM na pia Raisi wa zamani wa Austria, Kurt Waldheim. Risla ya KM wa sasa Ban Ki—moon juu ya msiba huo ilikumbusha ya kwamba Marehemu Waldheim alipata fursa ya kuutumikia UM kuanzia 1972 hadi 1981, katika kipindi ambacho, alitilia mkazo, ni muhimu sana katika historia ya taasisi hii ya kimataifa.

KM na wafanyabiashara waahidi mchango wao kukabiliana na UKIMWI

KM Ban Ki-moon pamoja na wafanyabiasahara wa sekta ya binafsi waliohudhuria kikao maalumu kilichofanyika Makao Makuu kuzingatia juhudi za kupiga vita UKIMWI, kifua kikuu na malaria wamethibitisha kwenye taarifa zao mbalimbali umuhimu na ulazima wa kuimarisha ushirikiano wa pamoja kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kuweza kudhibiti bora maradhi haya thakili yenye kusumbua umma wa kimataifa.