Habari Mpya

Hapa na pale

Tarehe 26 Juni huadhimishwa kuwa ni Siku ya Kimataifa dhidi ya Mateso, na kwenye risala ya KM Ban Ki-moon kuiheshimu siku hii walimwengu walikumbushwa wajibu wao katika kuwapatia tiba inayofaa waathiriwa wote wa mateso, kote duniani; na KM vile vile aliyahimiza Mataifa Wanachama kuuridhia haraka Mkataba wa Kimataifa dhidi ya Mateso.~

Jamii ya Shompole kupokea Zawadi ya Ikweta

Mnamo mwezi Januari 2002, Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) lilianzisha mpango maalumu uloikuwa na madhumuni ya kudumisha utunzaji wa viumbe anuwai na kuimarisha hifadhi ya mazingira, hasa kwenye zile sehemu za joto za tropiki.

Wenyeji wa asili watunza utamaduni wa kijadi kwa kutumia mawasiliano ya kisasa

Viongozi wa wenyeji wa asili walioshiriki kwenye mijadala ya kikao cha karibuni cha mwaka, cha Tume ya Kudumu ya UM juu ya Masuala ya Haki za Wenyeji wa Asili walisisitiza kwenye risala zao, kwa kauli moja, ya kwamba haiyafalii Mataifa Wanachama kuendelea kupoteza wakati katika kipindi cha kihistoria ambapo kunahitajika kuuidhinisha halan ule mwito wa Baraza la Haki za Binadamu wa kukomesha ubaguzi dhidi ya wenyeji wa asili, na kuupatia umma huu uliotengwa kijamii haki zao halali, hasa kwenye juhudi za kudhibiti na kutunza ardhi na rasilmali ziliopo kwenye maeneo yao.

Hali ya uchumi na jamii duniani kwa 2007

Ripoti ya UM juu ya Uchunguzi wa Hali ya Uchumi na Jamii Duniani kwa 2007 ilioelezewa kwa muktadha usemao \'Maendeleo katika Dunia yenye Kuzeeka\' iliwakilishwa wiki hii mbele ya waandishi habari wa kimataifa na Jose Antonio Ocampo, Makamu KM anayehusika na masuala ya uchumi na jamii. Ripoti iliashiria ya kuwa watu milioni 1.2 wenye umri wa miaka 60 na zaidi, watakuwa wanaishi kwenye mazingira ya hali iliokosa kile kinachojulikana kama ‘wavu wa hifadhi ya jamii’. Asilimia 80 ya fungu hili la umma wa kimataifa litakutikana zaidi katika mataifa yanayoendelea.

Siku ya Kuwakumbuka Wahamiaji Duniani

Ijumatano ya tarehe 20 Juni mwaka huu iliadhimishwa katika sehemu kadha wa kadha za ulimwengu kuwa ni ‘Siku ya Wahamiaji Duniani’, kumbukumbu zilizoshika fora katika kipindi ambapo pia kulitolewa mwito muhimu unaohimiza jumuiya ya kimataifa kukuza ushirikiano wao katika kuwasaidia wenziwao waliofurushwa makwao na kunyimwa makazi na maskani. Kadhalika mnamo siku hiyo kuliwasilishwa onyo lenye kuhadharisha walimwengu ya kwamba idadi ya wahamaji huenda kuongezeka katika kipindi kijacho.

Tume ya Baraza la Usalama imemaliza ziara ya wiki moja Afrika

Wajumbe 15 wanachama wa Tume ya Baraza la Usalama waliozuru mataifa matano ya Afrika kwa wiki moja walikamilisha ziara yao Ijumatano, tarehe 20 Juni katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) anbapo walifanya mazungumzo na watumishi wa UM waliopo huko pamoja na kuonana kwa mashauriano na Raisi Joseph Kabila na maofisa kadha wa Serekali.

KM na Baraza la Usalama kuyapongeza maafikiano ya amani Burundi

Raisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Juni, Balozi Johan Verbeke wa Ubelgiji aliwaambia waandishi habari kuwa wawakilishi wa Baraza hilo wanayaunga mkono maafikiano ya mazungumzo ya 17 Juni yaliokubaliwa Dar-es-Salaam, Tanzania baina ya Raisi wa Burundi Pierre Nkurunziza pamoja na kiongozi wa kundi la wanamgambo la Palipehutu-FNL, Agathon Rwasa.

Balozi mfadhili wa UNICEF aomba hifadhi bora kwa ama na watoto katika JKK

Lucy Liu, Balozi Mfadhili wa Shirika la UM juu ya Mfiuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), na ambaye vile vile ni mwigizaji maarufu wa michezo ya sinema katika Marekani juzi alitoa mwito maalumu karibuni baada ya kuzuru JKK ulioihimiza Serekali kuongeza juhudi zake za kuwapatia hifadhi bora na usalama watoto na wanawake raia walionaswa kwenye mazingira ya mapigano na uhasama.

Mazungumzo ya kuleta amani Sahara Magharibi kurudiwa tena Agosti

Mazungumzo ya siku mbili yaliodhaminiwa na UM, juu ya Sahara ya Magharibi, yaliofanyika wiki hii katika kitongoji cha Manhasset, New York kati ya Morocco na Chama cha Ukombozi wa Sahara ya Magharibi cha Frente Polisario, na ambayo vile vile yalijumuisha wawakilishi wa mataifa jirani na Sahara Magharibi ya Algeria na Mauritania, yalikamilishwa kwa makubaliano kuwa makundi husika yatarejea tena New York mnamo wiki ya pili ya Agosti kuendelea na majadiliano yao ya kutafuta suluhu ya kudumu na kuriidhisha juu ya mgogoro wa eneo hili la Afrika Kaskazini.

Sudan na UNMIS watakutana karibuni kuzingatia uboreshaji wa amani kusini

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani Sudan (UNMIS) na Serekali ya Sudan wanatazamiwa kukutana karibuni, kwenye kikao cha hadhi ya juu, kuzingatia njia za kuboresha utekelezaji wa maafikiano ya jumla ya amani ya 2005 yaliofuzu kusitisha vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe kati ya sehemu za kaskazini na kusini.