Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaotimuliwa kutoka nchi jirani ya Angola wanaendelea kuwasili nyumbani Congo, huku wengi wakiarifu kubughudhiwa ikiwa ni pamoja na kubakwa imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu nchini humo OCHA.
Chimbo la Ache nchini Indonesia limepiga hatua kubwa ya ujenzi mpya tangu kukumbwa na janga la tsunami miaka sita iliyopita. Hata hivyo ripoti ya Umoja wa Mataifa imeonya kwamba bado linakabiliwa na changamoto kubwa ya kuondoa umasikini, kuleta usawa na athari za majanga kwa siku zijazo.
Bodi kuu ya shirika la fedha duniani IMF juma hili imeidhinisha kuongezwa kwa muda wa miezi tisa wa kutoa mkopo kwa nchi ya Pakistan hadi mwezi Septemba mwaka 2011.
Msaada unaendelea kuwafikiwa maelfu ya wakimbizi wa ndani walioko katika kambi ya muda nje ya makao ya mpango wa Umoja wa Mataifa na wa Afrika wa kulinda amani Darfur UNAMID eneo la Kaskazini na Kusini mwa Darfur.
Mafuriko yanayoighubika Australia hivi sasa kwa mara nyingine yanaashiria umuhimu wa nchi zote zinazoendelea na zilizoendelea kuwa na mipango imara au la kukabiliwa na athari kubwa za hali ya hewa limesema shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na kupunguza majanga UNISDR.
Umoja wa Mataifa umezindua mchezo wa video kwa kutumia wavuti kwa lengo la kuwapa vijana taarifa muhimu kuhusu kuzuia maambukizi ya HIV, huku ukiwaelimisha, kuwaburudisha na kuchagiza tabia njema zinazojali afya zao.
Sehemu kubwa ya mavuno ya mpunga Kaskazini Magharibi mwa Haiti yatapotea kwa sababu wakulima wanahofia ugonjwa wa kipindupindu kwa mujibu wa shirika la chakula na kilimo FAO.
Ingawa misaada ya kibinadamu nchini Niger imeokoa maisha ya maelfu ya watoto wagonjwa, hali ya lishe bado inatia mashaka, ikiwa watoto 15 kati watoto 100 wanakabiliwa na utapia mlo uliokithiri.