Wanawake

Fafanuzi za Mjumbe wa Tanzania juu ya kikao cha Kamisheni ya CSW

Kamisheni ya UM juu ya Haki za Wanawake, au Kamisheni ya CSW ilifungua rasmi kikao cha mwaka, cha 52, mnamo Ijumatatu ya tarehe 25 Februari, kuzingatia masuala kadha kuhusu hadhi ya wanawake duniani, kufuatia mapendekezo yaliotolewa kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Beijing juu ya Wanawake, pamoja na yale maazimio ya kikao maalumu cha 23 cha Baraza Kuu la UM juu ya usawa wa kijinsiya na maendeleo ya wanawake kwa karne ya ishirini na moja.

KM ameanzisha rasmi kampeni ya kimataifa dhidi ya unyanyasaji wa wanawake

Asubuhi ya leo, Ijumatatu, Februari 25, KM wa UM Ban Ki-moon alianzisha rasmi kampeni ya kimataifa ya kukomesha na kufyeka tabia ya kutumia mabavu na nguvu dhidi ya wanawake na watoto wa kike duniani. Kampeni ilitilia mkazo umuhimu na ulazima wa kukomesha kidharura vitendo vyote vya udhalilishaji wa kijinsia. Kampeni hii imeanzishwa siku ile ile ambapo Kamisheni ya UM juu ya Haki za Wanawake (CSW)ilipfungua rasmi, kwenye Makao Makuu ya UM, kikao cha mwaka, cha 52. Tutakupatieni taarifa zaidi juu ya Mkutano wa CSW hapo kesho. ~

Hapa na pale

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kuwa ulimwengu unakabiliwa na ukosefu wa wahudumia afya milioni 4, na eneo lenye upungufu mkubwa zaidi ni bara la Afrika ambalo pekee linahitajia kidharura wafanyakazi milioni moja ziada ili kuweza kuyafikia malengo ya maendeleo na afya bora kama ilivyodhamiriwa na Nchi Wanachama. Kuanzia tarehe 2 hadi 7 Machi jumuiya ya kimataifa itakusanyika mjini Kampala, Uganda kuhudhuria mkutano wa kimataifa utakaojumuisha wataalamu wa serikali, wale wa kutoka sekta ya afya, vyuo vikuu na pia mashirika yasio ya kiserekali, ili kuzingatia hatua za kuchukuliwa kipamoja kusuluhisha tatizo la upungufu wa wahudumia afya duniani.

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu Duniani (UNIFEM) imeihimiza jamii ya kimataifa kuongeza juhudi za kukomesha kihakika, tabia hatari ya kutahiri watoto wa kike. UNIFEM imependekeza kwa nchi wanachama kuheshimu haki za wanawake pamoja na watoto wakike pote duniani, mwito ambao ulitangazwa Februari 7 (08) katika kipindi ambacho walimwengu walikuwa wakiiadhimisha na kuiheshimu Siku ya Kimataifa dhidi ya Ukeketaji wa Wanawake.

Watoto wadogo bado wanaendelea kuajiriwa kupigana

Ripoti mpya ya KM juu ya hali ya watoto katika maeneo yenye mapigano imebainisha kwamba kuna baadhi ya nchi wanachama ambazo bado zinaendeleza karaha ya kuwalazimisha watoto wadogo kujiunga na makundi ya wanamgambo na kushiriki kwenye mapigano. Mataifa haya, kwa mujibu wa ripoti ya UM, hujumuisha Afghanistan, Burundi, Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Colombia na vile vile Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Myanmar, Nepal, Philippines, Somalia, Sudan pamoja na Sri Lanka na Uganda.