Masuala ya UM

Kikao cha 63 cha Baraza Kuu kimefunguliwa rasmi Makao Makuu

Leo saa tisa alasiri kulifunguliwa rasmi kikao cha 63 cha Baraza Kuu la UM kwenye Makao Makuu yaliopo mjini New York, ambapo Miguel d’Escotto Brockmann wa Nicaragua alishika usukani wa uraisi wa Baraza hilo.

Hapa na Pale

Mashirika ya UM ya UNICEF, WHO na washiriki wanaohudumia misaada ya kiutu yamejumuika nchini Zimbabwe kukabili maradhi ya kipindupindu yalioripotiwa kuzuka katika vitongoji vya mji mkuu wa Harare, ambapo inaripotiwa watu 11 walifariki na 80 wengine waliambukizwa na maradhi hayo. UNICEF ikishirikiana kwa ukaribu zaidi na wenye madaraka wenyeji, pamoja na mashirika yasio ya kiserikali na WHO, imenzisha vituo viwili vya matibabu kuwasaidia wagonjwa wa kipindupindu. Zahanati hizo zinaendeshwa na lile shirika la madaktari wa kimataifa lijulikanalo kama Médecins Sans Frontières.

Hapa na Pale

~Shirika la UNAMID limeripoti ndege yao ya helikopta ilidungwa risasi Ijumapili katika eneo la Darfur Kaskazini na iliweza kutua salama na abiria ~12 pamoja na wafanyakazi 4 wa ndege, licha ya kuwa tangi la mafuta lilikuwa linavuja. UNAMID pia watumishi wake wawili walishambuliwa kwa risasi katika Darfur Magharibi na wahalifu wanaodaiwa kuwa wanamgambo wa Janjaweed waliokuwa wamevaa unifomu za kijeshi amabao walionekana karioibu na Makao Makuu ya Sekta ya Magharibi ya Kijeshi.~

Hapa na Pale

Raisi wa Baraza la Usalama kwa Septemba, Balozi Michel Kafando wa Burkina Faso, kwenye taarifa alioitoa baada ya mashauriano ya faragha juu ya hali katika JKK alieleza wajumbe wa Baraza wana wasiwasi na kuharibika kwa utulivu wa eneo la mashariki katika JKK, baada ya kuzuka mapigano ya karibuni kati ya vikosi vya Serikali (CAF) na kundi la waasi la CNDP. Baraza limesisitiza mapigano hayo yametengua maafikiano ya Goma yajulikanayo kama Actes ‘dEngagement de Goma na kusikitika kwamba walioridhia maafikiano hayo wanaonesha dharau na mapuuza ya ahadi walizotoa hapo kabla. Baraza limewataka wafuasi wa CNDP kukomesha haraka operesheni zao na linazingatia pia taarifa iliotolewa na kundi hilo ya kuahidi kuondosha vikosi vyao halan kutoka kwenye jukwaa la mapigano.

KM awasili kazini kwa gari ya nishati ya sola

KM leo asubuhi aliwasili kazini kwa gari maalumu yenye kutumia nishati ya sola, ambayo iliendeshwa kutokea nyumbani kwake mjini New York hadi jengo la Makao Makuu ya UM. Kadhia hii ni moja katika juhudi za KM za kuamsha hisia za umma wa kimataifa juu ya majukumu tuliyonayo kuhibiti bora mabadiliko ya hali ya hewa, na umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa kutumia teknolojia inayotunza mazingira hayo badala ya kuyadhuru.

Hapa na Pale

UM na mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu, yanayosimamia huduma za kuendeleza ilimu kwenye maeneo ya mgogoro Usomali, yametoa taarifa yenye kulaani vikali mashambulio ya karibuni dhidi ya majengo ya skuli, walimu na wanafunzi yaliofanyika katika mji wa Mogadishu.

HAPA NA PALE

Naibu KM Asha-Rose Migiro ameondoka New York Ijumatano kuelekea Lebanon kuhudhuria kikao cha 12 kilichotayarishwa na Baraza la Maendeleo ya Uchumi na Jamii kwa Asia ya Magharibi (ECOWAS) kitakachokutana kuanzia Septemba 13 hadi 14, 2008. Madhumuni ya mkutano ni kushauriana namna ya kusawazisha shughuli za mashirika ya UM ili kuimarisha mshikamano, kukuza ushirikiano na kujiepusha na tabia ya kurudufia kazi zao.

Hapa na Pale

Naibu KM Asha-Rose Migiro alipohutubia mjadala kuhusu tatizo la UKIMWI katika eneo la Afrika kusini ya Sahara alikumbusha kwamba janga hili ovu la UKIMWI “linamomonyoa” ustawi wa maendeleo yaliofikiwa baada ya uhuru, katika sehemu nyingi barani humo. Mkutano uliandaliwa bia na Chuo Kikuu cha UM pamoja na Chuo Kikuu cha Cornell, katika Jimbo la New York na ulifanyika kwenye ukumbi wa Dag Hammarskjöld wa Makao Makuu ya UM. Aliwahimiza wataalamu juu ya VVU/UKIMWI kulenga juhudi zao kwenye taaluma manufaa itakayowasilisha uamuzi wa vitendo utakaochangisha moja kwa moja kwenye vita dhidi ya maradhi maututi ya UKIMWI.

Hapa na pale

Ijumatatu, Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Huduma za Wahamiaji alihutubia kikao maalumu, cha mkutano wa mataifa wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya (EU) uliofanyika Paris kuzingatia suala la hifadhi ya kisiasa kwa watu wanaotoka nchi za nje. Mkutano huu uliitishwa na Ufaransa, taifa ambalo kwa sasa ndio linaloongoza uraisi wa EU. Kwenye risala yake Guterres aliyasihi mataifa ya EU yaendelee na juhudi zao za kujenga mfumo mpya, wenye uwazi na unaoeleweka, kukabiliana na suala la hifadhi ya kisiasa na utakaotumiwa na wote.

Hapa na Pale

Alkhamisi (04/09/08) alasiri Baraza la Usalama limepitisha taarifa mbili, moja ikisisitiza kwamba kunazingatiwa, kwa uangavu mkubwa, na wajumbe wa Baraza ile rai ya kupeleka vikosi vya ulinzi amani, vya kimataifa, Usomali katika siku za usoni kuchukua nafasi ya majeshi ya Umoja wa Afrika yaliopo huko hivi sasa. Kadhalika, taarifa iliyakaribisha mazungumzo, ya kiwango cha juu, ya kuunganisha tena taifa liliogawanywa miaka ya nyuma la Cyprus, baina ya raia wa Kigiriki na wale wa Kituruki.