Masuala ya UM

Taadhima ya Geneva inawakumbuka watumishi wa UM waliouawa Algiers

KM Ban Ki-moon, akijumuika na watumishi wa UM Geneva walifungua taadhima ya kuwaheshimu na kuwakumbuka wafanyakazi wenziwao 17 waliouawa na bomu la kujitolea mhanga Algeria mwezi uliopita, kwa kusimama kimya kwa dakika moja. Baada ya hapo KM alifunua rasmi ile bendera iliohifadhiwa ndani ya kioo kilichozungukwa na ubao wa matangazo, bendera ambayo ndio iliokuwa ikipeperuka kwenye ofisi za UM Algiers, na ilioraruliwa na kuchanwa na bomu la magaidi. KM alikabidhiwa bendera hiyo alipozuru ofisi za UM Algiers, siku chache baada ya tukio la magaidi kujiri.

KM ametangaza kumteua raia wa Mali kuwa Mshauri Maalumu kwa Afrika

Cheikh Sidi Diarra wa Mali ameteuliwa na KM Ban Ki-moon kuwa Mshauri mpya Maalumu kuhusu Masuala ya Afrika, na pia kuchukua wadhifa wa Mwakilishi Mkuu wa Nchi Masikini, Nchi Zisio Bandari pamoja na Nchi za Visiwa Vidogo Vidogo.

Mjumbe Mpya wa UM kwa Liberia amewasili kuanza kazi

Mjumbe Maalumu mpya wa KM kwa Liberia, Ellen Margrethe Loj wa Denmark amewasili Liberia kuanza kazi, na aemahidi kulisaidia taifa husika la Afrika Magharibi kuimarisha amani, utulivu na demokrasia katika kipindi cha mpito baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka kumi kusitishwa nchini. ~~Bi Loj alisema ijapokuwa mafanikio kadha yameshuhudiwa baada ya mapigano kusita, hata hivyo badio kuna majukumu mbalimbali yanayohitajia kushughulikiwa kuupatia umma wa Liberia utulivu wanaohitajia kuendeleza maisha yao ya kawaida.

Hapa na pale

Mnamo 2007 Shirika la Mfuko wa UM Kudhibiti Idadi ya Watu (UNFPA) limepokea mchango wa dola milioni 419 kutoka mataifa 181 kutumiwa katika kuongoza shughuli zake za mwaka, mchango ambao ulikiuka rikodi ya msaada uliopokewa miaka iliopita.

KM atathminia shughuli za UM kwa 2008

KM Ban Ki-moon alikutana na waandishi habari mwanzo wa wiki na aliwasilisha ajenda aliyopendekeza ijumuishwe katika kazi za UM katika mwaka 2008. KM Ban alisema kwenye risala yake ya ufunguzi kwamba atatumia wadhifa wake kuhakikisha 2008 utakaobarikiwa mchango ziada kutokana na bidii ya kimataifa katika kukabiliana na masuala yanayohusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani na pia ulinzi wa amani ya kimataifa.~~

Wajumbe elfu moja ziada wanahudhuria mkutano wa kurudisha amani Kivu

Mkutano uliodhaminiwa na UM kuzingatia uwezo wa kuudisha usalama, amani na maendeleo katika jimbo la mashariki la Kivu, kwenye Jamhuri ya Kideomkrasi ya Kongo (JKK) ulifungua mijadala yake mwanzo wa wiki mjini Goma, na mazungumzo haya yataendelea mpaka tarehe 17 Januari 2008.

2007 ulikuwa mwaka maututi hadi kwa watumishi wa UM duniani

Raisi wa Chama cha Watumishi wa UM, Stephen Kisambira aliripoti ya kuwa katika mwaka 2007 watumishi 42 wa UM waliuawa katika sehemu kadha za dunia wakati walipokuwa wanatekeleza wajibu wao wa kazi – idadi hiyo ilijumuisha vile vile wafanyakazi 17 waliouawa mnamo Disemba 11 na bomu la kujitolea mhanga katika mji wa Algiers, Algeria.

Operesheni za UNAMID katika Darfur zahitajia msaada ziada kidharura, asisitiza KM

Ripoti ya KM juu ya suala la kupeleka vikosi mseto vya UNAMID vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika Darfur imeonya kwamba mafanikio yaliojiri kwa sasa ni haba sana, na hayataviwezesha vikosi hivyo vya kimataifa kuyatekeleza majukumu yake kama ilivyodhaminiwa na Baraza la Usalama. Hali hii, alitilia mkazo, itaunyima umma wa Darfur utulivu na amani ya wa muda mrefu inayotakikana kidharura katika eneo lao.