Masuala ya UM

Hapa na pale

Mjumbe Maalumu wa KM juu ya Masuala ya Mgogoro na waasi wa LRA Uganda Kaskazini, Joaquin Chissano, Raisi wa zamani wa Msumbiji, amenakiliwa kuripoti kupatikana maafikiano ya kutia moyo mwisho wa wiki, baada ya Serikali ya Uganda na waasi wa LRA walipotiliana sahihi kwenye mji wa Juba, Sudan Kusini, mwafaka wa kudumisha kuacha kupigana.~

Hapa na pale

Edward Luck, raia wa Marekani ameteuliwa kuwa Mshauri Maalumu wa KM wa UM juu ya masuala yanayohusu hifadhi-kinga na misaada ya kiutu ya dharura penye uhasama wa kitaifa.

Mkutano wa kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa kufunguliwa Monaco

Kikao maalumu cha Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) kinafanyika sasa hivi Monaco kuzingatia sera mpya za kudhibiti bora mazingira kutokana na uharibifu unaochochewa na mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Mawaziri wa mazingira kutoka Mataifa Wanachama 100 ziada wanahudhuria mkutano.

Baraza la Usalama kujadili hali katika Usomali

Ijumatano Baraza la Usalama litazingatia hali katika Usomali na huenda likapitisha azimio juu ya vikosi vya ulinzi wa amani vya Umoja wa Afrika (UA).

Eritrea imezuia Walinzi wa usalama wa UM kuingia Ethiopia

Wenye madaraka Eritrea wamekataa kuwaruhusu watumishi wa Shirika la UM la Ulinzi wa Amani Mipakani Ethiopia/Eritrea (UNMEE) kwenda Ethiopia, hali ambayo iliwalazimisha kurejea mjini Asmara kusubiri ushauri kutoka UM juu ya hatua za kuchukuliwa nawo baada ya mvutano huu. Tukio la kuwazuia walinzi wa amani kutovuka mpaka limejiri licha ya kuwa Ijumaa iliopita Baraza la Usalama lilishtumu vikali "ukosefu wa ushirikiano" kutoka Serikali ya Eritrea, ambaye ililaumiwa kujitenga na majukumu yake ya kusaidia vikosi vya UNMEE kudhibiti bora usalama kwenye eneo la mgogoro mipakani.

Mjumbe wa vijana asailia kikao cha CSD juu ya maendeleo

Neema Buhile, ni mwakilishi wa Vijana wa Nchi za Jumuiya ya Madola kutokea Tanzania ambaye hivi majuzi alikuwepo hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UM) kuhudhuria kikao cha mwaka cha Kamisheni juu ya Maendeleo ya Jamii (CSD). Muktadha wa mkutano huo wa mwaka ulilenga zaidi yale masuala yanayofungamana na ajira, ulemavu, hali ya kuzeeka na pia vijana. Redio ya UM ilipata fursa ya kuzungumza na Neema ambaye alitupatia maoni yake kuhusu ushirikiano unaofaa kuendelezwa na wajumbe wa kimataifa ili kuyatekeleza mapendekezo ya vikao vya kimataifa, kama kikao cha mwaka CSD, kwa mafanikio. ~~Sikiliza mahojiano kamili kwenye idhaa ya mtandao.

Fafanuzi za Mjumbe wa Tanzania juu ya kikao cha Kamisheni ya CSD

Naibu KM Asha-Rose Migiro alifungua rasmi kikao cha 46 Kamisheni ya CSD wiki iliopita ambapo alitilia mkazo kwenye hotuba yake juu ya “jukumu muhimu la ajira na kazi stahifu katika kukuza maendeleo”, hususan kwenye nchi zinazoendelea. Ernest Ndimbo, Mkurugenzi wa Ajira kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Watoto Tanzania alikuwa miongoni mwa wawakilishi waliohudhuria mkutano wa Kamisheni ya CSD. Ndimbo alifanya mahojiano maalumu na Redio ya UM ambapo alichukua fursa hiyo kutupatia fafanuzi zake kuhusu kikao cha mwaka huu cha Kamisheni ya CSD.~

Baraza la Usalama lazungumzia hifadhi ya watoto wanaonaswa kwenye mazingira ya mapigano

Baraza la Usalama liliitisha kikao maalumu cha siku moja katika Makao Makuu, ambapo wajumbe kadha wa kadha walishauriana hatua za kuchukuliwa na Mataifa Wanachama ili kuwalinda watoto wenye umri mdogo dhidi ya vitimbi vya udhalilishaji, mateso na uonevu wanaokabiliwa nawo wakati wanapozongwa na mazingira ya migogoro na mapigano, unyanyasaji ambao umeonekana kukithiri katika miaka ya karibuni, hasa kwenye yale maeneo yalioghumiwa na kukumbwa na hali ya mapigano.~

UNAMID yaidhinisha na Sudan makubaliano kuhusu operesheni za amani Darfur

KM wa UM Ban Ki-moon ametangaza kufanikiwa kutia sahihi Maafikiano ya kuidhinisha Hadhi ya Vikosi Mseto vya UM/UA vinavyotazamiwa kulinda Amani katika Darfur, mapatano yatakayojulikana kama Maafikiano ya SOFA. Rodolphe Adada, Mjumbe Maalumu wa UM/UA wa Shirika la Ulinzi wa Amani kwa Darfur, UNAMID alitia sahihi Muwafaka huu pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Deng Alor.

Wasomali milioni mbili wahitajia haraka misaada ya kiutu

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imedhihirisha kwamba watu milioni 2 katika Usomali wanahitajia kufadhiliwa haraka misaada ya kiutu kutoka wahisani wa kimataifa ili kunusuru maisha.