Masuala ya UM

Ripoti ya KM yatathminia hali katika Usomali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon Ijumanne aliwasilisha ripoti mpya kuhusu hali katika Usomali. Ndani ya ripoti, Katibu Mkuu alieleza kwamba timu maalumu ya mashirika ya Umoja wa Mataifa, ikiongozwa na Idara ya Umoja wa Mataifa juu ya Masuala ya Kisiasa, ilishakamilisha makadirio ya sera mpya ya Umoja wa Mataifa yenye uwazi, na inayoeleweka, kuhusu uwezekano wa kupeleka vikosi vya ulinzi wa amani vya kimataifa nchini Usomali.

Dokezo ya ripoti ya OHCHR juu ya vurugu Kenya baada ya uchaguzi

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu (OHCHR) Ijumatano imetoa ripoti yenye kuelezea matokeo ya ziara ya wiki tatu Kenya, iliofanywa na wataalamu mwezi uliopita ambapo walichunguza kiini halisi cha machafuko na vurugu liliolivaa taifa hilo kufuatia uchaguzi wa Raisi katika Disemba 27, 2007.~

Mazungumzo ya Sahara Magharibi yamekhitimisha duru ya nne mjini New York

Duru ya nne ya mazungumzo ya siku mbili kuzingatia suala la Sahara ya Magharibi imemaliza mijadala yake Ijumanne katika wilaya ya Manhasset, kwenye jimbo la New York. Vikao viliongozwa na Mjumbe wa KM kwa Sahara ya Magharibi, Peter van Walsum, na kuhudhuriwa na wawakilishi wa Morocco, Chama cha Ukombozi cha Frente Polisario pamoja na wajumbe kutoka mataifa jirani ya Algeria na Mauritania.

BU lazingatia tatizo la ugaidi dhidi ya amani ya kimataifa

Ijumatano Baraza la Usalama limekutana kwenye mkutano wa hadhara, kuzingatia azimio linalohusu vitisho vinavyochochewa na vitendo vya kigaidi, dhidi ya usalama na amani ya kimataifa. Baraza lilitazamiwa baadaye kupiga kura ya kupitisha azimio juu ya suala hili.~

Arbour kuyahimiza mataifa yaridhie Mkataba wa Kuondosha Ubaguzi Duniani

Louise Arbour, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu Duniani ametoa mwito maalumu kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kufyeka Ubaguzi, mwito ambao umependekeza kwa Mataifa Wanachama kuidhinisha haraka ule Mkataba wa Kimataifa wa 1969 wa Kuondosha Aina Zote za Ubaguzi Ulimwenguni, na kujitahidi kuimarisha sheria zao kitaifa ili kuhakikisha waathiriwa wa janga la ubaguzi huwa wanapatiwa haki. Siku ya Kimataifa Kuondosha Ubaguzi huadhimishwa kila mwaka na jamii ya UM katika tarehe 21 Machi.~

Mashauriano ya wapatanishi wa UM/UA kwa Darfur yamemalizika Geneva

Wajumbe Wapatanishi wa Umoja wa Mataifa (UM) na Umoja wa Afrika (UA) kwa Darfur, yaani Jan Eliasson na Salim Ahmed Salim, Ijumanne mjini Geneva walimaliza mashauriano yao ya siku mbili, yasio rasmi, pamoja na washirika wenzi wa kieneo na pia waangalizi wa kimataifa.

KM ahutubia Mkutano wa OIC

KM wa UM Ban Ki-moon leo alihudhuria Mkutano wa siku mbili wa Umoja wa Nchi za KiIslam (OIC) unaofanyika mjini Dakar, Senegal. Kwa mujibu wa Msemaji wa UM, KM Ban aliwasili Dakar Ijumatano ambapo alikutana kwa mashauriano na KM wa Umoja wa OIC, Ekmeleddin Ihsanoglu na walishauriana juu ya uwezekano wa kuyasuluhisha yale matatizo yanayohusu Kosovo, ukaliaji mabavu wa Israel katika maeneo ya WaFalastina, pamoja na kusailia matatizo ya ugaidi, chuki za kibaguzi dhidi ya WaIslam, na vile vile kuzingatia suala la uhuru wa mawazo na kujieleza.~

'Ufunguo wa kuyafikia Malengo ya Milenia umo mikononi mwa wanawake', anasihi NKM

Mapema wiki hii, Naibu KM wa UM, Asha-Rose Migiro aliwahutubia wanachama wa Baraza la Marekani juu ya Uhusiano wa Kimataifa (Council on Foreign Relations) liliopo mjini New York, ambapo alisailia mada iliotilia mkazo kaulimbio isemayo ‘wanawake ndio wenye ufunguo wa kuyafikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs)kwa wakati na kupunguza umasikini na hali duni kwa nusu, itakapofika 2015.”

Hapa na pale

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu Geneva, imetangaza ya kuwa Louise Arbour ameamua kustaafu mwezi Juni atakapomaliza miaka minne ya mkataba wake wa kazi. Arbour angelipendelea kuendelea kuongoza ofisi hiyo, na kuwakabili kinaga naga wale wakosoaji dhidi yake, lakini alisema anaaamini wakati umefika kushughulikia zaidi mahitaji ya familia yake sasa hivi.

Ban Ki-moon apongeza juhudi za upatanishi za Kofi Annan Kenya

Ijumanne KM Ban Ki-moon alipokuwa Geneva, kabla ya kurejea New York, alikutana na KM Mstaafu Kofi Annan, ambaye alimpongeza kwa juhudi zake muhimu zilizosaidia kuleta suluhu ya kuridhisha juu ya ule mzozo ulioselelea Kenya kwa miezi miwili kufuatia uchaguzi.