Masuala ya UM

KM ahutubia Mhadhara wa Geneva, atathminia athari za mfumko wa bei za chakula duniani

Ijumanne KM Ban Ki-moon alihutubia, kwa mara ya awali, mhadhara mpya unaojulikana kama Mhadhara wa Geneva, ambapo alizungumzia hatari inayokabili umma wa kimataifa kutokana na kuenea, kwa mapana na marefu, kwa lile tatizo la kupanda kwa kasi kwa bei za chakula duniani.

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kwamba matokeo ya utafiti wa karibuni yamethibitisha asilimia 4 tu ya wahamiaji wa Iraq waliopo Syria, waliohajiri makwao kwa sababu ya vurugu wapo tayari kurejea nchini kwao. Asilimia 95 ya wahamiaji hawa waliihama Iraq kutokana na vitisho pamoja na ukosefu wa usalama kijumla.

Wakariri wa haki za binadamu wana wasiwasi na hali Zimbabwe

Wakariri sita wa UM wanaohusika na haki za binadamu wamenakiliwa wakisema wana wasiwasi kuhusu kuporomoka kwa haki za binadamu na kuzuka kwa hali ya mtafaruku Zimbabwe kufuatia uchaguzi wa raisi na bunge uliofanyika March 29. Wataalamu hawa wanahusika na masuala ya mauaji ya kihorera, udhalilishaji wa wanawake, haki ya kupata makazi, haki ya uhuru wa kusema na hifadhi kinga dhidi ya mateso. Kwenye ripoti iliotolewa Geneva wataalamu hawo walibainisha kwamba wamepokea ripoti zenye kuaminika, zilizoelezea ya kuwa tangu uchaguzi ulipomalizika nchini Zimbabwe, vitendo vya vitisho na uonevu vilikithiri dhidi ya wale raia waliodhaniwa na kutuhumiwa kupigia kura, au kuunga mkono, chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) na wale waliohusika na Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC).

KM ameshtumu mauaji katika Tarafa ya Ghaza

KM Ban Ki-moon ameshtumu upotezaji wa maisha ya raia uliotukia mapema Ijumatatu kwenye Tarafa ya Ghaza, msiba ambao pia ulisababisha vifo kadha, ikijumuisha vifo vya mama mmoja na watoto wake wanne. Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na Ofisi ya KM kuhusu tukio hili, vikosi vya Israel vilivyokuwa vikiendeleza operesheni zake katika Ghaza vilikumbushwa tena dhamana walionayo, chini ya sheria za kiutu za kimataifa, ya kuhifadhi na kuwahami raia walionaswa kwenye mazingira ya mapigano.

Msemaji wa KM asisitiza, tuhumu dhidi ya walinzi wa amani katika JKK zinapotosha

Naibu Msemaji wa KM, Marie Okabe, kwenye mazungumzo na waandishi habari Ijumatatu, alikanusha madai ya ripoti za Shirika la Habari la Uingereza la BBC, kwamba walinzi wa amani wa UM katika JKK wameshiriki kwenye biashara ya magendo nchini humo.

ILO inasema udhibiti bora makazini huokoa maisha

Shirika la UM juu ya Haki za Wafanyakazi (ILO) limetoa ripoti mpya yenye kuonyesha watu milioni 2.2 hufariki kila mwaka katika dunia kwa sababu ya ajali zinazoambatana na ajira pamoja na maradhi wanayopata makazini. ILO imependekeza taratibu za usimamizi kwenye mahali pa kazi zirekibishwe ili kuwawezesha viongozi na mameneja kutambua na kubashiria mapema zaidi hatari ziliopo na kuzidhibiti mapema kabla hazijasababisha vifo vya ajali.

UM inawakumbuka watumishi waliofariki wakihudumia bodi la kimataifa

Tarehe ya leo Aprili 25 inaheshimiwa hapa Makao Makuu kama Siku Maalumu ya Kuwakumbuka Wafanyakazi wa UM waliopoteza maisha wakati wakitumikia taasisi hiyo ya walimwengu. Katika taadhima zilizofanyika kwenye bustani ya Makao Makuu, waandishi habari wenziwetu kutoka Redio ya UM, Geraldine Adams na Jerome Longue walisoma orodha ya majina ya wafanyakazi 294 waliofariki tangu Disemba 2005.

Mjumbe wa Afrika Mashariki kwenye UNCTAD XII asailia kikao

Wajumbe kadha kutoka Mataifa Wanachama wa UM walikusanyika katika mji mkuu wa Accra, Ghana kuhudhuria kikao cha 12 cha Taasisi ya UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ambacho kilifunguliwa rasmi Aprili 20, na mijadiliano yaliendelea karibu wiki moja. Mkutano Mkuu wa UNCTAD hufanyika kila baada ya miaka minne. Dhamira ya kikao cha mwaka huu cha 12 ilikuwa kuzingatia taathira zinazoletwa na huduma za msawazisho wa lazima wa shughuli za uchumi katika soko la kimataifa, au kwa lugha nyengine kuzingatia taathira ya marekibisho yaliochochewa na mfumo wa utandawazi.

UM kuiadhimisha rasmi Siku ya Malaria Duniani

Kikao cha 60 cha Baraza Kuu la Shirika la Afya Duniani (WHO), kilichofanyika Geneva mwezi Mei 2007, kilipitisha, kwa kauli moja pendekezo la kuifanya tarehe 25 Aprili kila mwaka iadhimishwe kuwa ni Siku ya Malaria Duniani. Makusudio ya pendekezo hili ni kuitumia siku hiyo kupigia mbiu ya mgambo zile juhudi za kimataifa za kudhibiti bora ugonjwa maututi wa malaria. ~

KM ametoa ripoti mpya kuhusu udhibiti wa silaha ndogo ndogo

Ripoti mpya ya KM kuhusu Udhibiti wa Silaha Ndogo Ndogo Duniani iliotolewa rasmi wiki hii imehimiza kuanzishwe haraka mashauriano ya karibukaribu miongoni mwa Mataifa Wanachama juu ya suala hili, utaratibu ambao anaamini ndio wenye uwezo pekee wa kusaidia kuendeleza vizuri zaidi juhudi za kujikinga na athari zinazoletwa na silaha ndogo ndogo. KM alipendekeza Mashauriano ya Ratiba ya Utendaji yafufuliwe, na yapewe umuhimu wa hali ya juu ili kudhibiti bora matumizi ya silaha ndogo ndogo duniani. Kadhalika KM alilitaka Baraza la Usalama liwe linahusishwa zaidi kwenye zile juhudi za kuimarisha vikwazo dhidi ya matumizi ya silaha ndogo ndogo.