Masuala ya UM

KM kuyakaribisha maafikiano ya Serikali ya Vyama Vingi Kenya

KM wa UM Ban Ki-moon, kwa kupitia msemaji wake, ameripoti kukaribisha kwa furaha tangazo la Raisi wa Kenya, Mwai Kibaki juu ya maafikiano ya kuunda Serikali Kuu ya Vyama Vyingi, hususan vile vyama vilivyohusika moja kwa moja na mzozo uliofumka Kenya baada ya uchaguzi.

UNICEF itashindwa kuhudumia watoto chakula baada ya bei za nafaka kuongezeka

Kadhalika, Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limetangaza kwamba kwa sababu ya kupanda kwa bei za chakula duniani, shirika litashindwa kuhudumia chakula watoto katika seghemu mbalimbali za dunia, hasa wale wanaoishi katika mataifa yanayoendelea, watoto ambao kawaida hutegemea kukirimiwa misaada ya chakula kutoka mashirika ya kimataifa kwa madhumuni ya kujikinga na tatizo kuu la utapia mlo.

KM apendekeza mifumko ya bei za chakula idhibitiwe haraka

Kwenye hotuba aliowasilisha hapo jana kwenye kikao kilichoandaliwa na Baraza la ECOSOC pamoja na taasisi za Bretton Woods ~ yaani Benki Kuu ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani ~ na kujumuisha pia Shirika la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) na Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO), KM Ban alitoa mwito maalumu ulioyakumbusha Mataifa Wanachama kwamba kunahitajika kuchukuliwe hatua za haraka, za muda mfupi na muda mrefu, kuhakikisha tatizo la mgogoro wa bei za chakula duniani linadhibitiwa kidharura.

Taasisi za kimataifa na ECOSOC zinazingatia Makubaliano ya Monterrey

Baraza la UM juu ya Maendeleo ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) ikijumuika na taasisi za Bretton Woods – yaani Benki Kuu ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF) – na ikichanganyika pia na Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) na Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) leo wamefanyisha hapa Makao Makuu kikao cha siku, cha hadhi ya juu kujadiliana ushirikiano wa kuchukuliwa na Mataifa Wanachama, kuyatekeleza Makubaliano ya Monterrey, kwa taratibu zitakazodhibiti bora miradi ya maendeleo duniani.

Fafanuzi za Mjumbe wa Vatikana kuhusu ziara ya Papa Benedict XVI katika UM

Kiongozi wa Wakristo wa madhehebu ya Kikatoliki, Papa Benedict XVI anatarajiwa kuzuru Makao Makuu ya UM, Ijumaa ijayo, tarehe 18 Aprili.

Ripoti ya KM inapongeza juhudi za kuleta suluhu ya kudumu katika JKK

Ripoti mpya ya KM juu ya hali katika JKK imethibitisha kwamba hatua muhimu zilichukuliwa karibuni nchini ili kuharakisha juhudi za kuwasilisha suluhu ya kudumu kwenye eneo la wasiwasi la mashariki, licha ya kuwa vizuizi kadha wa kadha viliibuka hapa na pale katika shughuli za amani.

KM ameanza ziara rasmi katika Shirikisho la Urusi

KM Ban Ki-moon leo ameanza rasmi ziara ya siku tatu kwenye Shirikisho la Urusi ambapo anatarajiwa kusailia na viongozi wa taifa hilo, wakijumuisha Raisi Vladimir Putin pamoja na Raisi Mteule Dmitry Medvedev, masuala yanayohusu hali katika Kosovo, na mpango wa amani juu ya Mashariki ya Kati, hasa ilivyokuwa Urusi imependekeza kuandaa mkutano maalumu wa kuzingatia suala hilo.

KM anayaomba Mataifa Wanachama kuunga mkono mageuzi katika UM

KM Ban Ki-moon leo asubuhi aliwasilisha risala muhimu kwenye mjadala maalumu wa Baraza Kuu kuzingatia uwezekano wa kuleta mageuzi bora kwenye usimamizi wa kazi na shughuli za UM, sio katika Makao Makuu pekee bali vile vile kwenye mashirika yake kadha wa kadha yaliozagaa katika sehemu mbalimbali za dunia.

IAEA kutathminia usalama wa viwanda vya nyuklia kwenye vikao vitatu tofauti

Shirika la UM juu ya Huduma za Amani za Nishati ya Nyuklia (IAEA) linatarajiwa Ijumatano, tarehe 09 Aprili, kuanzisha vikao vitatu tofauti kutathminia usalama wa viwanda vinavyozalisha nishati za nyuklia ulimwenguni. Vikao hivi vitajumuisha wataalamu wa kutoka vyuo vikuu, viongozi wa viwanda vya kimataifa na vile vile magwiji wanaohusika na mashirika yanayosimamia matumizi salama ya viwanda vya nyuklia.

Siku ya Kumbukumbu ya Mauaji ya Rwanda kuheshimiwa Makao Makuu

Leo magharibi, tarehe 07 Aprili KM wa UM Ban Ki-moon atatoa risala maalumu ya kuwakumbuka wale raia walioangamizwa Rwanda miaka 14 iliopita kutokana na jinai ya mauaji ya halaiki. KM anatarajiwa kuikumbusha jumuiya ya kimataifa kuhusu dhamana ya maadili waliokabidhiwa nayo na umma, ya kuunga mkono, kwa kauli moja, juhudi za UM za kuzuia janga karaha la mauaji ya halaiki kuibuka tena ulimwenguni. Kwa mujibu wa takwimu za UM watu 800,000 ziada waliangamia Rwanda na waathiriwa kadha wengineo walionusurika na mauaji walidhurika kiakili. KM ameahidi ya kuwa ataendelea kutumia muda wa utumishi wake katika UM kuhakikisha walimwengu tunafanikiwa kuuzuia milele hatari ya mauaji ya halaiki kuibuka tena duniani.