Masuala ya UM

Hapa na Pale

Ndege ya helikopta iliokodiwa na UM kuhudumia Vikosi vya Mchanganyiko vya UM/UA kwa Darfur (UNAMID) iliripotiwa kuanguka na kuharibiwa kabisa ilipoanza kuruka kutoka Nyala, mji mkuu wa Darfur Kusini. Wahudumu wanne wa helikopta hiyo walifariki. Marie Okabe, msemaji mshiriki wa KM, aliwaambia waandishi habari ya kwamba ripoti za awali zilizopokewa na UM zimethibitisha ndege yote iliteketea. Taarifa ziada zinatarajiwa kutangazwa baada ya UNAMID kumaliza uchunguzi kamili kuhusu ajali.~

Hapa na pale (Taarifa za Kusoma)

Mohamed ElBaradei, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) Ijumatatu aliwaambia wajumbe wa Bodi la Magavana wa taasisi waliokutana Vienna, kwamba wakaguzi wake wameweza kuthibitisha Iran haijabadilisha matumizi ya nyuklia kinyume na dhamira ilioripotiwa nao. Kadhalika ElBaradei alisema IAEA haikufanikiwa kuthibitisha madai ya baadhi ya mataifa kwamba mradi wa nishati ya nyuklia wa Iran, unafungamana na shughuli za kijeshi. Aliyataka yale Mataifa Wanachama yenye kudai kuwa na ushahidi mradi wa Iran wa nyuklia hutumiwa kwenye shughuhuli za siri za kijeshi yaipatie IAEA ushahidi huo ili uthibitishwe na wataalamu wake kama ni ushahidi wa kweli au la.

UM unaadhimisha Siku ya Amani Kimataifa

Umoja wa Mataifa unaadhimisha Siku ya Amani Kimataifa kwa kuandaa tafrija kadha wa kadha zilienedelezwa katika Makao Makuu mjini New York, na kwenye maeneo mengine ya dunia. KM Ban Ki-moon alijumuika na watu mashuhuri kadha walioteuliwa kama Wajumbe wa Amani wa UM, pamoja na Raisi wa Baraza Kuu na watumishi wa UM kwenye tafrija maalumu ya kila mwaka ambapo KM aligonga kengere ya amani iliopo kwenye bustani ya UM.

Hapa na Pale

Vikosi vya Ulinzi Amani vya UM katika JKK (MONUC), vikisaidiwa na helikopta za vita Ijumaa walishambulia wafuasi wa kundi la waasi wa CNDP kwenye mji uliopo eneo la mashariki, kilomita 60 kutoka mji wa Goma. Waasi hao walikuwa wanaelekea jimbo la Kivu Kaskazini kwa madhumuni ya kuuteka mji baada ya kutangaza kabla dhamira yao hiyo. Shambulio la vikosi vya MONUC liliwalazimisha kurudi nyuma na kukatiza lengo lao.~~

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuunga mkono huduma za kusaidia watoto maskini 155,000, wanaohudhuria skuli za msingi 883, kupata mlo wa kila siku kwenye jimbo la Toliara nchini Bukini. Krystyna Bednarska, mwakilishi mkazi wa UNICEF-Bukini, alisema mradi huu utaiwezesha Bukini kukamilisha, kwa wakati, lile lengo la MDGs la kuwapatia watoto wote, wanaume na wanawake, ilimu ya msingi. Serikali ya Bukini imeshachangisha dola milioni 2.4 kuhudumia mradi huo.

Raisi mpya wa BK ahimiza demokrasia ihuishwe katika UM

Raisi mpya wa Baraza Kuu la UM, Miguel D’Escoto Brockmann, aliyekuwa Waziri wa Nchi za Nje wa Nicaragua, jana jioni alifungua rasmi kwenye Makao Makuu ya UM kikao cha 63 kinachojumuisha Mataifa Wanachama 192 kutoka kila pembe ya dunia, ambapo wajumbe wao hukusanyika kila mwaka, kuanzia mwezi Septemba hadi Disemba, kuzingatia masuala yote muhimu ya kimataifa, na kuchukua maamuzi kwa kulingana na kanuni za Mkataba wa UM.

Srgjan Kerim ana matumaini mema juu ya mageuzi katika BU

Raisi aliyepita wa kikao cha 62 cha Baraza Kuu, Srgjan Kerim, ambaye alimaliza muda wake Ijumatatu, (15/09/08) alipokutana na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu hapo jana, alibainisha ya kuwa kulipatikana mafanikio makubwa kwenye kazi za Baraza, chini ya uongozi wake, hasa pale wajumbe wa kimataifa waliporidhia kuzingatia uwezekano wa kurekibisha na kuleta mageuzi kwenye mfumo wa Baraza la Usalama.

Hapa na Pale

Baraza la Usalama lilikutana asubuhi, kwenye kikao cha faragha, kushauriana juu ya masuala ya usalama na amani katika bara la Afrika. Kwenye mashauriano ya asubuhi Baraza lizingatia taarifa kuhusu mzozo wa karibuni kati ya Eritrea na Djibouti, ripoti ambayo iliwakilishwa mbele ya wajumbe wa Baraza hilo na Joaõ Honwana, Mkurugenzi wa Kitengo cha Afrika katika Idara ya UM juu ya Masuala ya Kisiasa (DPA). Kadhalika, Baraza liliilia “mada nyenginezo” ambazo hatujadhihirishiwa hasa zinahusika na nini.

Kikao cha 62 cha Baraza Kuu kimekamilisha shughuli zake

Ijumatatu usiku kikao cha 62 cha Baraza Kuu la UM kilikamilisha shughuli zake kwa kupitisha maazimio kadha. Moja ya azimio muhimu liliopitishwa mkutanoni, kwa kauli moja, ni lile pendekezo la kuanzisha tena, kabla ya tarehe 28 Februari mwakani, majadiliano ya kupanua uwanachama wa Baraza la Usalama. Azimio hili lilipitishwa baada ya mivutano ya saa nyingi kati ya wawakilishi wa kutoka Mataifa Wanachama.~

Kikao cha 63 cha Baraza Kuu kimefunguliwa rasmi Makao Makuu

Leo saa tisa alasiri kulifunguliwa rasmi kikao cha 63 cha Baraza Kuu la UM kwenye Makao Makuu yaliopo mjini New York, ambapo Miguel d’Escotto Brockmann wa Nicaragua alishika usukani wa uraisi wa Baraza hilo.