Masuala ya UM

Uchaguzi wa uraisi Zimbabwe sio halali, anasema KM

KM Ban Ki-moon, kwenye taarifa iliotolewa kwa kupitia msemaji wake, amelaumu na kushtumu matokeo ya uchaguzi wa uraisi uliofanyika Zimbabwe mwisho wa wiki iliopita, uchaguzi ambao alisisitiza umekosa uhalali chini ya hsreia ya kimataifa.

Hapa na pale

Naibu KM wa UM Asha-Rose Migiro, kwenye risala alioitoa mbele ya wajumbe waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Afrika unaofanyika Sharm el-Sheikh, Misri kuanzia Ijumatatu amepongeza uamuzi wa kuingizwa mada inayohusu Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwenye ajenda yao - hususan lile saula la kuyapatia mataifa yanayoendelea usafi wa mastakimu na maji salama.

Nchi wanachama zahimizwa kuidhinisha mkataba dhidi ya mateso

Tarehe ya leo, Juni 26, inaheshimiwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Ushikamano na Waathiriwa wa Mateso, siku ambayo KM aliitumia kutoa mwito unayoyahimiza Mataifa Wanachama wa UM kuidhinisha haraka Mkataba dhidi ya Mateso, na pia kuridhia Itifaki ya Khiyari ya Mkataba huo ambao hujumuisha pendekezo la kuchunguza, bila ya vizuizi, vituo vya kufungia watu vya kitaifa na kimataifa, ili kutathminia utekelezaji wa haki za wafungwa. ~

KM anajiandaa kuzuru Asia

KM Ban Ki-moon anatarajiwa kuanza ziara ya siku 12 katika bara la Asia kuanzia kesho Ijumaa ambapo pia atahudhuria Mkutano Mkuu wa Mataifa Wanachama wa Kundi la G8 utakaofanyika Ujapani.

Hapa na pale

Baraza la Usalama, kwenye taarifa ya raisi kwa mwezi Juni, limeyasihi makundi yote yanayohasimiana Sudan Kusini kutumia mwongozo wa \'ramani ya mapatano\' yaliofikiwa Juni 8 kwenye yale Maafikiano ya Jumla ya Amani, ili kuzima cheche za fukuto liliozusha fujo za karibuni kwenye mji wa Abyei.

BU kushtumu fujo na utumiaji mabavu Zimbabwe

Ijumatatu usiku, Baraza la Usalama liliafikiana, kwa kauli moja, kushtumu kampeni ya utumiaji mabavu inayoendelezwa na wenye madaraka Zimbabwe, dhidi ya wapinzani wa kisiasa, na pia kulaani vitendo vya Serikali ambavyo inaripotiwa huwanyima wapinzani haki ya kuendeleza kampeni huru za uchaguzi. Kwenye taarifa iliotolewa baada ya majadiliano ya faragha katika Baraza la Usalama, Raisi wa mwezi Juni wa Baraza, Balozi Zalmay Khalilzad wa Marekani alisema wajumbe wa Baraza wanaamini fujo iliotanda sasa hivi Zimbabwe, ikichanganyika na vikwazo dhidi ya vyama vya upinzani, ni hali ambayo uchaguzi ulio huru na wa haki hauwezekani kufanyika abadan, uchaguzi ambao umetayarishwa ufanyike Juni 27 (2008).

UNHCR inashinikiza mfanyakazi aliotekwa nyara Usomali aachiwe

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kuwa linaendelea kushinikiza, kwa sauti kuu, aachiwe huru yule mfanyakazi wao, Hassan Mohammed Ali, ambaye alitekwa nyara Ijumamosi iliopita kutoka nyumbani kwake katika mji wa Afgooye, kilomita 30 kutoka Mogadishu, na watu wasiojulikana. Kwa mujibu wa UNHCR mateka Ali aliweza kuzungumza kwa simu na aila yake Ijumapili usiku na alisema hali yake ni nzuri; lakini taarifa nyengine ziada yoyote kuhusu mahali alipo na utambulisho wa makundi yaliomtorosha haijulikani. ~

Hapa na Pale

Baraza la Usalama limekutana kusailia na kushauriana juu ya operesheni za Shirika la UM linalosimamia usitishwaji wa mapigano mipakani Ethiopia na Eritrea (UNMEE), na pia kuzingatia hatua za kuchukuliwa siku za mbele na jamii ya kimataifa kuhusu ulinzi wa eneo hilo.

Zawadi ya UM juu ya Huduma za Jamii kutunzwa taasisi 12 za kimataifa

Tarehe 23 Juni huadhimishwa kila mwaka na UM kuwa Siku ya Kuheshimu Mchango wa Huduma za Umma Kimataifa. Jamii ya kimataifa, kwa kuiadhimisha siku hiyo, ilizitunukia taasisi 12 za kimataifa Zawadi ya 2008 ya UM Kuhusu Huduma za Umma, taasisi ambazo kwa mchango wao kwenye huduma za kijamii zilifanikiwa kufaidisha maisha mema kwa watu wa kawaida wanaoishi kwenye maeneo yao.

Siku ya Wahamiaji Duniani Inaadhimishwa Kimataifa

Tarehe 20 huadhimishwa kila mwaka kimataifa, kuwa ni Siku ya Wahamiaji Duniani – siku ambayo umma wa kimataifa huheshimu na kukumbushana juu ya jukumu liliodhaminiwa Mataifa Wanachama na Mkataba wa UM kuhudumia kihali na mali umma wenziwao uliong\'olewa kwa nguvu makwao kwa sababu wasioweza kuzidhibiti. Kadhalika mnamo siku hiyo walimwenngu huheshimu mchango wa wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa wanaoshughulikia ugawaji wa misaada ya kiutu kwa wahamiaji hawo.