Masuala ya UM

UM waadhimisha miaka 62 tangu Mkataba kuthibitishwa

Alkhamisi, 24 Oktoba (2007) iliadhimishwa duniani kote kuwa ni ‘Siku Kuu ya Kuzaliwa UM’. Miaka 62 iliopita, mnamo tarehe 24 Oktoba 1945 Mkataba wa UM uliidhinishwa na kuanza kutumika kimataifa.

KM amewasilisha bajeti la dola bilioni 4.2 kujadiliwa na Baraza Kuu

Kadhalika Alkhamisi KM Ban Ki-moon aliwakilisha kuzingatiwa mbele ya Baraza Kuu bajeti la kuendesha shughuli za UM katika miaka miwili ijayo liliogharamiwa dola bilioni 4.2

Mwakilishi mpya wa KM kwa Sudan kawasili Khartoum

Ashraf Jahangir Qazi, Mwakilishi Maalumu mpya wa KM kwa Sudan, ambaye pia ni mkuu wa Shirika la Ulinzi wa Amani la UM Sudan (UNMIS), amewasili Khartoum wiki hii na kutarajiwa kufanyisha msururu wa mikutano na maofisa wa ngazi ya juu wa Serikali, akiwemo vile vile Raisi wa Sudan Omar AlBashir na pia Makamu wa Kwanza wa Raisi na Raisi wa Serikali ya Sudan Kusini, Salva Kiir.

KM ana wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa raia Kivu Kaskazini

KM wa UM Ban Ki-moon ameripoti kuingiwa wasiwasi mkuu juu ya athari kwa raia kutokana na uharibifu wa hali ya utullivu Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Taarifa alizopokea KM zilionesha kukithiri kwa mateso dhidi ya umma raia, ambapo watu huwa wanafukuzwa makwao na unyanyasaji wa kijinsia kuongezeka. Hali hii ilisababishwa na mapigano KivuKaskazini kati ya vikosi vya Serikali na makundi ya wanamgambo na wanajeshi waasi, wafuasi wa Jenrali mtoro Laurent Nkunda.~~

Mkurugenzi wa UNDP asifu maendeleo ya uchumi Afrika kusini ya Sahara

Kemal Dervis, Mkurugenzi Msimamizi wa UNDP karibuni alifanya ziara ya siku 10 katika Msumbiji, Rwanda na Tanzania. Aliporejea Makao Makuu aliitisha mkutano na wanahabari wa kimataifa katika mwanzo wa wiki na alielezea kwamba ule mfumo wa kuambatanisha utekelezaji wa miradi ya mashirika ya UM chini ya mwongozo mmoja, kitaifa, unatekelezwa kwa taratiibu zenye kutia moyo sana katika zile nchi alizozitembelea.

Walimwengu watambua mchango wa watu wazee katika maendeleo

Tarehe 01 Oktoba iliadhimishwa na UM kuwa ni ‘Siku Kuu ya Watu Wenye Umri Mrefu/Watu Wazee’ na kulitolewa mwito maalumu ulioyahimiza mataifa yote wanachama kuandaa miradi ya kizalendo, kwa dhamira ya kuwapatia umma wa kimataifa wenye umri wa miaka 60 na zaidi, wanaotafsiriwa kama watu wazee, pensheni ya kudumu maridhawa itakayowasaidia kuishi vizuri kama raia wengine wenziwao.

Baraza Kuu lakhitimisha mjadala wa mwaka na kuhimiza kuwepo vitendo badala ya maneno

Mjadala wa kikao cha 62 cha wawakilishi wote ulioshtadi katika ukumbi wa Baraza Kuu, mjini New York, kuanzia tarehe 25 Septemba, ulikamilishwa na kutiwa kikomo Ijumatano tarehe 03 Oktoba. Kabla ya mijadala kuanza wajumbe kutoka nchi 191 wanachama walitatarajiwa kuwasilisha sera zao kuhusu uhusiano wa kimataifa. Baada ya mijadala kukamilishwa wawakilishi kutoka mataifa 189 ndio waliosajiliwa kumudu kuzungumzia kikao.

Ghana kuongoza Baraza la Usalama kwa mwezi Oktoba

Ghana imekabidhiwa uraisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Oktoba. Mwakilishi wa Kudumu wa Ghana katika UM, Balozi Leslie Kojo Christian aliitisha mkutano wa waandishi habari wa kimataifa katika Makao Makuu ambapo aliwaarifu kuhusu ajenda ya vikao vijavyo kwa mwezi Oktoba. Balozi Christian alidhihirisha ya kuwa ajenda ya mijadala italenga zaidi yale matatizo yanayohusu hali katika Usomali na Cote d’Ivoire, na pia alitarajia kusailiwa masuala juu ya haki za wanawake, pamoja na mada zinazoambatana na juhudi za kimataifa za kuimarisha usalama na amani duniani.

KM na jamii ya kimataifa walaani mauaji ya wanajeshi wa AU Darfur

KM Ban Ki-moon, akiungwa mkono na maofisa kadha wa vyeo vya juu katika UM, ameshtumu vikali mauaji ya wanajeshi wanaolinda amani wa Umoja wa Afrika Sudan (AMIS), yaliofanyika mwisho wa wiki iliopita katika mji wa Haskinita, Darfur Kusini.