Masuala ya UM

Ziara ya faragha ya KM katika Iraq

KM Ban Ki-moon Alkhamisi alifanya ziara ya fargha ya siku moja katika Iraq. Wakati alipokuwa huko alikutana kwa mazungumzo, mjini Baghdad na Waziri Mkuu Nouri Kamal al-Maliki na kuzungumzia juu ya mchango wa UM katika kuusaidia umma wa Iraq kurudisha utulivu wa amani na maendeleo kwenye taifa lao.

Mapendekezo ya KM kurekebisha shughuli za UM yaungwa mkono na Baraza Kuu

Baraza Kuu la UM Alkhamisi limepitisha maazimio mawili muhimu ya kuunga mkono mapendekezo ya KM Ban Ki-moon ya kuleta mageuzi katika kazi za taasisi hii muhimu ya kimataifa. Azimio la kwanza linalenga Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani (DPKO), na limekusudiwa kuboresha kazi za Idara kwa kuipatia uwezo wa kupeleka haraka vikosi vya UM kulinda amani kwenye maeneo yenye machafuko. Vile vile azimio limetaka kubuniwe Kitengo cha Idara juu ya Huduma za Amani Nje ya Makao Makuu.

Ban Ki-Moon ana matumaini amani kurejea tena Uganda kaskazini

KM Ban ameripoti wiki kuwa na mataraji ya kutia moyo kwamba hali ya utulivu na amani itarejea tena katika Uganda ya Kaskazini, kutokana na juhudi za Joaquim Chissano, Mjumbe Maalumu wa KM kwa maeneo yalioathirika na mapigano na waasi wa kundi la LRA.