Sheria na Kuzuia Uhalifu

'Msiba mwengine wazuka Ghuba ya Aden': UNHCR

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kuwa imejumuika na washiriki wengine wa kimataifa kuwatafuta wahamiaji karibu 100 wanaoripotiwa kupotea katika Ghuba ya Aden, baada ya kulazimishwa na wafanya magendo kuchupa kutoka kwenye chombo walichokuwemo, nje ya mwambao wa Yemen.

Ngirabatware amekana makosa ya jinai ya halaiki Rwanda

Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) imeripoti ya kwamba Augustin Ngirabatware, aliyekuwa Waziri wa Mipango ya Nchi Rwanda Ijumaa alipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza kukabili mashitaka alikana makosa kumi ya kushiriki kwenye mauaji ya halaiki nchini mwao katika miaka ya 1990, jinai ambayo inasemekana ilikiuka sheria ya kiutu ya kimataifa.

Waziri wa zamani Rwanda ahamishiwa kizuizini Arusha

Waziri wa zamani wa Miradi ya Nchi Rwanda, Augustin Ngirabatware, anayekabili mashitaka ya kushiriki kwenye mauaji ya halaiki na ukiukaji mbaya wa kanuni za kiutu za kimataifa, Ijumatano amehamishwa kutoka Frankfurt, Ujerumani, alipokamatwa wiki mbili zilizopita, na kupelekwa kwenye Kituo cha Kufungia Watu cha Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) kilichopo Arusha, katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu ahimiza hifadhi bora kwa wageni Afrika Kusini baada ya mauaji katili

Navanethem Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu (OHCHR), amelaani vikali mauaji ya kikatili yaliotukia Ijumaaa iliopita katika kijiji cha Eastern Cape, Afrika Kusini ambapo Sahra Omar Farah, mama wa KiSomali pamoja na watoto wake wawili wa kiume wajane, ambao mmoja wao alikuwa kiziwi, na vile vile binti wake wa miaka 12 waliuawa kikatili kwa visu na marungu karibu na duka liliokuwa linaendeshwa na Msomali.

IOM itapanua huduma za kuokoa watoto waliotoroshwa Afrika Magharibi

Shirika la Kimataifa juu ya Wahamaji (IOM) limetangaza leo kwamba litapanua zaidi mradi wa kusaidia kurejesha makwao wale watoto waliotekwa nyara Afrika Magharibi, na ambao hushirikishwa kwenye kazi za kulazimisha katika nchi za kigeni. Mradi huu ulianzishwa mwaka 2006, na unafadhiliwa na Idara ya Masuala ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Mwendesha Mashtaka wa ICC awasiliana na viongozi wa kimataifa juu ya Darfur

Luis Moreno Ocampo, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai ya Halaiki (ICC) yupo New York kwa madhumuni ya kuwasiliana na watendaji wa kimataifa – yaani UM na wawakilishi wa Afrika – kuhusu taratibu za kuwapatia raia wa Darfur hifadhi ziada na kukomesha vitendo vya uhalifu dhidi yao na kuhakikisha maamuzi na madaraka ya Mahakama juu ya suala hilo yanatekelezwa haraka kwenye eneo la mtafaruku la Sudan magharibi.

Nchi 17 zakubali mapendekezo ya kudhibiti kisheria vitendo vya makampuni ya wanajeshi wa kukodi

Wataalamu kutoka nchi 17 waliokutana kwenye kikao maalumu kwenye mji wa Montreux, Uswiss kuanzia Ijumatatu (15/09/08), kuzingatia udhibiti bora wa shughuli za yale makampuni ya wanajeshi wa binafsi wanaohudumia usalama, hii leo wamepitisha warka maalumu uliosisitiza ya kuwa Serikali za Mataifa zina dhamana kuu ya kuhakikisha askari wakandarasi wa binafsi wanaokodiwa kushiriki kwenye maeneo ya uhasama na vita huwa wanafuata sheria za kiutu za kimataifa.

Matumizi ya madawa ya usanisi yameshuhudiwa kuongezeka katika nchi zinazoendelea, UNODC yaripoti

Ofisi ya UM juu ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC) imebainisha kwenye ripoti ya \'Tathmini ya 2008 juu ya Madawa ya Kulevya Yanayotumiwa kama Viburudisho Duniani\' kwamba matumizi ya yale madawa ya usanisi ya anasa – kama "amphetamine, metamphetamine (meth) na ecstasy" – yamebainika kuzidi katika nchi zinazoendelea, hasa katika maeneo ya Mashariki na Kusini-Mashariki ya Bara la Asia na katika Mashariki ya Kati.

UM umeitisha mjadala maalumu kusikiliza hisia na maoni ya waathiriwa wa ugaidi duniani

Hii leo, kwenye Makao Makuu ya UM mjini New York, kumeanzishwa mjadala maalumu wa kihistoria, ulioandaliwa na KM Ban Ki-moon mwenyewe, ambao umewakusanyisha waathiriwa wa vitendo vya ugaidi kutoka sehemu kadha za kimataifa na kuwapatia fursa ya kuelezea hisia zao juu ya misiba waliopitia, kwa madhumuni ya kuwakilisha taswira ya kiutu kwa waathiriwa wa janga la ugaidi duniani.

Usafirishaji wa magendo warejea tena kwenye Ghuba ya Aden

Baada ya kurudi kwa hali shwari kwenye Ghuba ya Aden imeripotiwa na hirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) kuanza tena, upya, mnamo mwezi Agosti, usafirishaji magendo wa wahamiaji waliokuwa wakijinusurisha na njaa pamoja na mapigano katika eneo la Pembe ya Afrika, hususan wahamiaji kutoka Usomali na Ethiopia.